Thursday, May 08, 2025

NHC YATWAA JENGO LA UBIA MJINI MOROGORO LILILOCHELEWESHWA UJENZI KWA MIAKA 17

  Jengo la ghorofa sita lililopo Kiwanja Na. 67/I, barabara ya zamani ya Dar es Salaam mjini Morogoro kabla halijawekewa uzio.


Jengo hilo la ghorofa sita lililopo Kiwanja Na. 67/I, barabara ya zamani ya Dar es Salaam mjini Morogoro baada ya kuwekewa uzio.
Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Bw. Muungano Saguya akizungumza na Waandishi wa HAbari Mjini Morogoro.
Mpangaji wa jengo hilo Jane Lucas akizungumza na Waandishi wa Habari


Katibu wa wapangaji wa jengo hilo, Emil Mshana akizungumza na waandishi wa habari.

Mmoja wa mafundi akipigilia misumari kuweka uzio katika jengo hilo.

Morogoro

Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limechukua hatua madhubuti ya kulinda maslahi ya wananchi na usalama wa jengo la ghorofa sita lililopo Kiwanja Na. 67/I, barabara ya zamani ya Dar es Salaam mjini Morogoro, kwa kusitisha matumizi ya jengo hilo na kurejesha usimamizi wake rasmi baada ya kucheleweshwa kukamilika kwa takribani miaka 17.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia ukiukwaji mkubwa wa masharti ya mkataba wa ubia kati ya NHC na kampuni ya M/S Saze & Samo Investment Ltd, inayoongozwa na mwekezaji Sameer Ismail maarufu kwa jina la Lotto.

Akizungumza na waandishi wa habari, Meneja Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Bw. Muungano Saguya alisema kuwa mkataba wa ubia ulisainiwa mwaka 2007 kwa lengo la kuendeleza jengo la kisasa kwa manufaa ya wakazi wa Morogoro, kwa miaka miwili, lakini utekelezaji wake ulikumbwa na changamoto nyingi zilizotokana na kutokuzingatia taratibu za kisheria na kitaalamu.

"Mbia alishindwa kufuata taratibu za msingi za ujenzi kama vile kutumia wataalamu waliothibitishwa, kupata vibali halali vya ujenzi, pamoja na kutozingatia viwango vya usalama," alieleza Saguya.

Aidha, licha ya kupewa maelekezo na onyo mbalimbali na NHC, mbia huyo aliendelea na ujenzi bila kufuata ushauri wa kitaalamu. Hatimaye, mnamo Septemba 27, 2023, Shirika lilirejesha rasmi usimamizi wa mradi huo na kuweka ulinzi katika eneo hilo kwa ajili ya usalama wa wananchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya tathmini ya kiufundi iliyotolewa na Kitengo cha Ushauri wa Ujenzi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (BICO), ilibainika kuwa jengo hilo lilikuwa na kasoro kubwa za kiusalama. BICO ilishauri ujenzi usiendelee zaidi ya ghorofa ya tatu, lakini mbia aliendelea na kazi kinyume cha ushauri huo na bila kibali kutoka Manispaa ya Morogoro wala NHC.

NHC imesisitiza kuwa hatua hii inalenga kuhakikisha kuwa jengo hilo linakamilika kwa ubora unaokubalika, kwa kutumia wataalamu wake wenye uzoefu na weledi wa hali ya juu.

"NHC pia itazingatia uwekezaji uliofanywa na mbia na kuchukua hatua stahiki za fidia kwa mujibu wa sheria na masharti ya kimkataba," alisema Saguya.

Kwa upande wao, wapangaji waliokuwa wakitumia jengo hilo wameiomba Serikali kupitia NHC kuhakikisha kuwa maboresho ya jengo hilo yanatekelezwa haraka ili waweze kurejea kuendesha shughuli zao za kiuchumi.

Katibu wa wapangaji, Emil Mshana, alisema kuwa jengo hilo limekuwa ni sehemu ya maisha yao kwa zaidi ya miaka 16 na limewasaidia kuendesha biashara zao, wengi wao wakiwa wanategemea mikopo ya kibiashara.

"Tumeathirika sana. Tulitegemea angalau taarifa ya mapema ili tuweze kupanga mikakati mbadala. Lakini tunatambua umuhimu wa usalama, na tunaomba maboresho yafanyike haraka," alisema kwa masikitiko.

Mpangaji mwingine, Bi. Jane Lucas, alisema alishangazwa kukuta jengo limefungwa bila taarifa ya awali na sasa hana pa kupeleka vifaa vyake vya biashara.

"Hapa kuna watu wamechukua mikopo na tegemeo lao ni hizi biashara. Tunaiomba NHC itusaidie kurahisisha mchakato wa kurejea baada ya maboresho," aliongeza.

NHC kupitia sera yake mpya ya usimamizi wa miradi ya ubia iliyozinduliwa Novemba 2022, imeongeza uwajibikaji kwa wabia. Hadi sasa, miradi saba imekamilishwa kwa mafanikio, minne imerejeshwa kwa Shirika, na wabia sita wamepewa notisi kwa kuvunja masharti ya mikataba.

Shirika hilo limewataka wabia wote kuwa waaminifu na kufuata taratibu za ujenzi, huku likitoa rai kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika miradi ya maendeleo kwa kuzingatia sheria, viwango na usalama wa jamii.

Mwekezaji wa jengo hilo, Bw. Sameer Ismail, hakupatikana kutoa maoni licha ya juhudi kadhaa za kumtafuta kufanyika.

NHC imeahidi kuendelea kusimamia kwa weledi miradi yote ya maendeleo nchini, ili kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, salama na yanayochochea ukuaji wa uchumi katika maeneo yao.

No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO ATEMBELEA KAMPUNI YA KIMATAIFA YA VIFAA TIBA NCHINI ITALIA

ROMA, ITALIA – Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango, ametembelea kampuni ya kimataifa ya uzalis...