Monday, September 09, 2013

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Bernard Membe Akutana na Waandishi wa Habari Jijini Dar es Salaam Nakusema:''Serikali ya Tanzania haijamfukuza mtu yeyote nchini mwenye sifa za ukiimbizi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.''

 Mhe. Bernard K. Membe (Mb), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa jana alikutana na waandishi wa habari katika ofisi za Wizara ya Mambo ya Nje mjini Dar es Salaam.  Katika mazungumzo yake, Mhe. Waziri Membe alielezea yaliyojiri katika Mkutano wa Wakuu wa Nchi wa Sekretarieti ya Maziwa Makuu (ICGLR) uliofanyika mjini Kampala, Uganda hivi karibuni. 
 Mhe. Waziri Membe akiendelea kuongea na waandishi, wakati Balozi Vincent Kibwana, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa akisikiliza kwa makini. 
 Mhe. Waziri Membe akiongea na waandishi wa habari.
 Balozi Dora Msechu (kulia), Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Amerika katika Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Omari Mjenga, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia katika Wizara ya Mambo ya Nje nao wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe. 
Balozi Celestine Mushy (kushoto), Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Bw. Elibariki Maleko (kulia), Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya Mambo ya Nje wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe.  
 Waandishi wa habari wakimsikiliza Mhe. Waziri Membe wakati wa mazungumzo nao jana.Picha na Reginald Philip na Tagie Daisy Mwakawago-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa
---
Na Ally Kondo

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa Mhe. Bernard K. Membe (Mb) ameuambia Umma wa Tanzania na dunia kwa ujumla kuwa Serikali ya Tanzania haijamfukuza mtu yeyote nchini mwenye sifa za ukiimbizi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Mhe. Waziri aliyasema hayo alipokutana na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 06 Septemba, 2013.

“Serikai haikumfukuza mkimbizi yeyote isipokuwa iliwafukuza wahamiaji haramu, Aidha, wahamiaji haramu hao walipewa onyo la kuondoka nchini na wengi wao wametii kabla ya operesheni maalum ya kuwatia mbaroni haijaanza” Waziri Membe alisikika akisema.

Kuhusu hoja kuwa operesheni ya kuwafukuza wahamiaji haramu inawalenga Wanyarwanda, Waziri Membe alisema kuwa hoja hiyo sio ya kweli. Alisema kuwa hadi kufikia wakati huu zaidi ya wahamiaji haramu 31,000 wameondoka nchini. Kati ya hao Warundi ni 21,000, Wanyarwanda ni 6,000 tu na waliobaki ni kutoka nchi nyingine..

Mhe. Membe aliwaambia waandishi wa habari kuwa Tanzania imekuwa kimbilio la wakimbizi kwa muda mrefu na hadi sasa inahifadhi wakimbizi zaidi ya laki 4. Wakati wote wakimbizi wamekuwa wakipewa huduma nzuri na haijawahi kusikika kuwa Tanzania inalaaniwa na Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa au Jumuiya ya Kimataifa kwamba Serikali inawanyanyasa wakimbizi.

Sambamba na taarifa hiyo, Mhe. Waziri aliwaambia waandishi wa habari kuhusu mikutano inayofanywa na baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (Kenya, Uganda na Rwanda) bila kuhusisha nchi nyingine wanachama wa jumuiya hiyo.

Mhe. Membe alisema kuwa yeye binafsi hana tatizo na mikutano hiyo endapo tu, imepata kibali cha Wakuu wa Nchi wa EAC pamoja na kutoa ripoti ya masuala yanayozungumzwa katika vikao vya jumuiya. “Mimi binafsi sioni tatizo kwa nchi hizo kukutana endapo zimepewa Baraka na Wakuu wote wa Nchi wa EAC na ripoti za mikutano yao kuwasilishwa katika vikao rasmi vya jumuiya” alisema Mhe. Membe.

Aliwatoa shaka Watanzania kutokuwa na hofu na mikutano hiyo kwa kuwa Tanzania ni nchi muhimu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, hivyo hainabudi nchi nyingine kuitegemea kutokana na rasilimali zilizopo  na jiografia yake.

Alihitimisha mazungumzo yake kwa kusema kuwa anaamini vikao vinavyofanywa, vinafanywa kwa nia njema pasipo kuwa na dhamira ya kuleta mgawanyiko ndani ya jumuiya. Na endapo vinafanywa kwa dhamira ya kuleta mgawanyiko basi muda wa kurekebisha hali hiyo upo. 

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...