Kongamnao kuhusu Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote na Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Mpango wa Ufadhili wa Sekta ya Afya yanafanyika kwenye Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha jijini Arusha kuanzia tarehe 29 na 30 Oktoba 2024 na 31 Oktoba na 01 Novemba 2024 mutawalia.
Matukio
hayo mawili yatakayofunguliwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) siku ya tarehe 30 Oktoba
2024 yamekusanya wataalamu kutoka sekta mbalimbali wa ndani na nje ya
nchi kujadili mikakati inayofaa kutumiwa na nchi za Jumuiya ya Afrika
Mashariki kuboresha huduma za afya kwa wote.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa
kushirikiana na Wizara ya Afya, Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika
Mashariki na wabia wa maendeleo imeshiriki uratibu wa maandalizi ya
matukio hayo muhimu ambapo Mdahalo wa Kitaifa kuhusu Mpango wa Ufadhili
wa Sekta ya Afya, kufanyika kwake ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la
Kisekta la Mawaziri wa Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki wakati wa
kikao chao kilichofanyika jijini Dar Es Salaam mwezi Mei 2024.
Aidha, mdahalo huo ni utekelezaji wa maazimio ya Wakuu wa Nchi
na Serikali wa Umoja wa Afrika waliyoyatoa katika Mkutano wao
uliofanyika jijini Addis Ababa, Ethiopia Julai 2019.
Katika siku yake ya kwanza, washiriki wa kongamano hilo walipata
fursa ya kusikiliza mada mbalimbali zilizokuwa zinawasilishwa na
watalaam wa afya. Kabla ya mada hizo kuanza kuwasilishwa, zilitanguliwa
na hotuba fupi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu na
Mkurugenzi wa Sera na Mipango katika Wizara ya Afya, Bw. Amoury A.
Amoury. Watalaamu hao waliwambia washiriki madhumuni ya kongamano hilo
na matokeo yanayotarajiwa na dira ya mpango wa bima ya afya kwa wote
nchini Tanzania.
Mada nyingine zilizowasilishwa katika siku ya kwanza ni pamoja
na Kugharamia Mfumo wa Afya kwa Wote: Kuangalia kwa kina mikakati ya
kibunifu kwa ajili ya Upatikanaji Endelevu wa Fedha; (Financing
Universal Health: Exploring Innovative Strategies for Sustainable
Funding in Tanzania); Nafasi ya Teknolojia na Ubunifu katika Kuboresha
Ufanisi na Upatikanaji wa Huduma ya Bima ya Afya kwa Wote; (Role of
Technology and Innovation in Improving Access and Efficiency in
Universal Health Insurance); na Enrolment and Re-enrolment Strategies –
what works and what does not work.
Wizara inawakilishwa na timu ya watalaamu katika kongamano hilo
inayoongozwa na Mkurugenzi wa Miundombinu ya Uchumi na Huduma za Jamii,
Mhandisi Abdillah Mataka na siku ya ufunguzi, Naibu Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya
Afrika Mashariki, Mhe. Denis Londo (Mb) atashiriki hafla ya ufunguzi ya
matukio hayo.
No comments:
Post a Comment