Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi, amesema kwa mikakati ya kutangaza Utalii inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, hakuna jambo litakalozuia kufikiwa kwa lengo la watalii milioni 5 ifikapo mwaka 2025.
Dkt. Abbasi ameyasema hayo Oktoba 28, 2024, alipokuwa akitoa mada kuhusu hali na maendeleo ya sekta ya utalii nchini Tanzania ikiwa moja ya sekta muhimu kwa maendeleo ya watu na ulinzi wa Taifa kwa washiriki wa Kozi Fupi ya 13 inayoendelea kwenye Chuo cha Ulinzi cha Taifa (NDC), jijini Dar es Salaam.
Kozi hiyo inahusisha washiriki kutoka nchi zaidi ya 20 duniani wengi wakiwa kutoka mabara ya Afrika na Asia.
Ameeleza mikakati kama filamu ya “Tanzania: The Royal Tour” na “Amazing Tanzania” na ushirikishaji wa sekta binafsi wakiwemo wadau wenyewe wa utalii katika kuitangaza nchi kuwa ni mambo ambayo nchi nyingine za Afrika na dunia zinaweza kujifunza kutoka Tanzania.
Ametoa wito pia kwa wataalamu hasa kutoka Bara la Afrika kuja na mikakati ya pamoja kulitangaza Bara hilo (Brand Africa Strategy) na kuhakikisha amani na usalama vinashamiri kwani sekta ya utalii, pamoja na jitihada za nchi na nchi, kukosekana kwa usalama katika nchi moja kunaweza kulifanya Bara zima kama la Afrika kuonekana ni la migogoro na hivyo kuathiri ujio wa wageni hata katika nchi zenye amani.“Ulikuwa wakati mujarabu kujadiliana na wabobezi hao na kubadilishana uzoefu wa nchi mbalimbali katika sekta ya utalii, uchumi na ulinzi wa Taifa. Wengi wao wameeleza kujifunza mengi kutoka mikakati na mafanikio makubwa ambayo Tanzania imeyafikia katika utalii, uhifadhi na zaidi ulinzi wa raslimali za Taifa,” amesema Dkt. Abbasi.
Comments