Utalii wa Puto Ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha: Mpango Mzima wa Kuinua Sekta ya Utalii






Na Happiness Shayo

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb), leo Oktoba 7, 2024, amezindua rasmi utalii wa puto katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya hifadhi hiyo. Uzinduzi huu umefanyika katika eneo la Korongo View ndani ya hifadhi, mkoani Iringa, ukiashiria hatua mpya katika kuvutia watalii na kukuza sekta ya utalii nchini Tanzania.

Utalii wa puto, maarufu kwa watalii wa kimataifa, unalenga kutoa uzoefu wa kipekee wa kutazama mandhari ya kuvutia ya Ruaha kutoka angani. Hifadhi hii ni maarufu kwa wanyamapori wake, wakiwemo tembo, simba, na wanyama wengine wa porini, ambao sasa watalii wanaweza kuwaangalia kutoka juu kwa kutumia puto. Mpango huu unatarajiwa kuimarisha utalii na kuvutia wageni wapya, hasa wale wanaotafuta uzoefu wa kipekee.

Akizungumza katika mahojiano maalum kupitia Kipindi cha Jambo Tanzania cha Shirika la Utangazaji la TBC, Mhe. Chana alieleza mafanikio haya kama matokeo ya jitihada za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye ameendelea kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania kimataifa. "Tunamshukuru Rais Samia kwa kuionesha dunia uzuri wa vivutio vyetu, jambo ambalo limepelekea ongezeko kubwa la watalii, kufikia milioni 1.8 na kuongeza mapato ya Taifa kwa asilimia 17%," alieleza Mhe. Chana.

Aliongeza kuwa sekta ya utalii sasa inachangia takribani dola za kimarekani bilioni 3.6 kwa mwaka kupitia fedha za kigeni, huku serikali ikiendelea kufanya maboresho makubwa katika miundombinu ya hifadhi mbalimbali. Katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, Waziri Chana alibainisha kuwa ujenzi wa barabara ya Iringa-Msembe yenye urefu wa kilomita 104 utaanza hivi karibuni. Vilevile, Serikali ina mpango wa kujenga uwanja wa ndege ndani ya hifadhi hiyo ili kurahisisha usafiri wa watalii, sambamba na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Nduli uliopo Iringa.

Mhe. Chana alihitimisha kwa kuwahimiza wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza kwenye sekta ya utalii, hasa katika Hifadhi ya Taifa Ruaha, ambayo inaonyesha fursa nyingi zinazoweza kuleta mafanikio makubwa kwa taifa. Alisisitiza kuwa katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, sekta ya utalii imepiga hatua kubwa, na serikali itaendelea kuboresha maeneo mengine ya vivutio vya utalii ili kuhakikisha sekta hii inazidi kuimarika na kutoa ajira kwa wananchi wengi zaidi.

 

Comments