Dar es Salaam, Oktoba 29, 2024 – Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefungua rasmi Mkutano wa 11 wa Merck Foundation Africa Asia Luminary katika Hoteli ya Johari Rotana, jijini Dar es Salaam. Mkutano huu unaleta pamoja viongozi, wenza wa wakuu wa nchi, watunga sera, wanataaluma, watafiti, na wanahabari kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika na Asia, wakiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano katika masuala ya afya, hasa afya ya uzazi, saratani, na magonjwa yasiyoambukiza.
Akizungumza kabla ya ufunguzi rasmi wa mkutano huo, Rais Dkt. Samia alikutana na baadhi ya wenza wa wakuu wa nchi kutoka nchi 15 za Afrika na Asia waliokuja nchini Tanzania kwa ajili ya kushiriki mkutano huu muhimu. Mhe. Rais alisisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano wa kimataifa katika kuimarisha mifumo ya afya kwa ustawi wa jamii, akitilia mkazo msaada unaotolewa na Merck Foundation kwa kuwajengea uwezo wataalamu wa afya ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazokabili sekta ya afya.
Mkutano huu wa siku mbili ni wa kipekee kwani unawaleta pamoja viongozi na wadau wa afya na maendeleo, wakiwemo Mawaziri wa Afya, watafiti, na wanahabari kutoka mataifa mbalimbali, kwa lengo la kubadilishana maarifa na kujadili mikakati ya kuboresha afya barani Afrika na Asia. Mhe. Dkt. Samia aliwakaribisha washiriki wote kwa furaha kubwa na kueleza kuwa Tanzania inaendelea kutekeleza sera na mipango ya kuboresha sekta ya afya, ikiwemo kuimarisha huduma za afya vijijini na mijini kupitia uwekezaji wa miundombinu na mafunzo kwa wataalamu wa afya.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Merck Foundation, Dr. Rasha Kelej, alielezea shukrani zake kwa Tanzania kwa kuwa mwenyeji wa mkutano huu na kupongeza jitihada zinazofanywa na Rais Samia katika kuimarisha afya ya umma. Alibainisha kuwa Merck Foundation ina lengo la kusaidia mafunzo ya taaluma za afya kwa kuendelea kushirikiana na nchi mbalimbali kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa watu wote.
Mkutano huu wa Merck Foundation Africa Asia Luminary umehitimishwa kwa mikakati na mapendekezo muhimu yatakayosaidia kuimarisha afya ya jamii kwa kuzingatia mahitaji ya kiafya ya watu kutoka mabara ya Afrika na Asia.
No comments:
Post a Comment