Mwenyekiti wa Kamati ya Wapangaji wa Kariakoo, Bw. Shafiq Mohamed,wakati wa kikao cha Kamati ya Wapangaji na Shirika la Nyumba la Taifa na baadhi ya wapangaji wa zamani wa NHC.
Dar es Salaam, Oktoba 2024 – Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limetoa tamko rasmi kwamba halijamtuma dalali yeyote kusimamia upangaji wa majengo mapya yanayojengwa kwa ushirikiano na wabia katika maeneo mbalimbali, ikiwemo Kariakoo. Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah, alitoa kauli hiyo wakati wa kikao cha Kamati ya Wapangaji na baadhi ya wapangaji wa zamani, kufuatia malalamiko kutoka kwa wafanyabiashara wakidai madalali wamekuwa wakitumia majengo hayo kujinufaisha, huku wakidai Shirika halihusiki na fedha zinazokusanywa.
Mkurugenzi Mkuu aliahidi kwamba NHC itaendelea kuboresha mazingira ya biashara na kuhakikisha haki za wapangaji zinalindwa ili kuondoa changamoto zilizopo na kutekeleza miradi ya ubia kwa manufaa ya pande zote. Aidha, aliweka wazi kuwa wapangaji wanaotarajiwa kurejea kwenye majengo ya zamani hawatakuwa na uhakika wa kurudi kwenye nafasi walizokuwa nazo, kwani upangaji mpya utazingatia mipangilio ya sasa na mahitaji mapya.
Katika hatua nyingine, Shirika limeamua kuwa vibao vidogo vya matangazo vilivyowekwa na wapangaji havitatozwa ada, lakini mabango makubwa yatatozwa kwa mujibu wa viwango vilivyowekwa na NHC, TRA, na Tanroads. Vilevile, wapangaji waliokwenda mahakamani kufungua kesi dhidi ya NHC wamepoteza haki ya upangaji wa majengo hayo.
Shirika limeahidi kuweka wazi michoro ya majengo mapya ya ubia kwa kamati ya wapangaji, na kufanikisha mipango ya kuwapatia wapangaji na wabia ushirikiano wa karibu na mipango endelevu.
Akizungumza kwa niaba ya wapangaji, Mwenyekiti wa Kamati ya Wapangaji wa Kariakoo, Bw. Shafiq Mohamed, aliishukuru NHC kwa kusikiliza maoni yao na kuahidi kuendelea kushirikiana na kamati katika kupanga mipango endelevu. Hata hivyo, wafanyabiashara wameeleza kuwa vizimba na sehemu zilizotengwa ni ndogo ikilinganishwa na maduka ya awali, hali inayoweza kuathiri biashara zao. Walieleza matumaini yao kuwa Shirika litaweka mpango bora wa kuwapa mazingira rafiki ya biashara.
Changamoto nyingine ni malalamiko kuhusu madalali kupewa nguvu zaidi katika usimamizi wa majengo hayo, jambo lililoleta migogoro kati ya wapangaji na wabia. Takribani wapangaji 437 wameeleza kuwa wanahitaji msaada wa Mkurugenzi Mkuu ili kuboresha mazingira ya biashara.
Kwa upande wa malipo ya ada za mabango, NHC ilibainisha kuwa suala hilo litajadiliwa ili kuweka uwazi wa ada hizo kwa wapangaji na kuondoa migogoro. Pia, wapangaji wameomba waruhusiwe kuingia kwenye majengo yanapokuwa yamekamilika kwa sehemu kubwa, badala ya kusubiri mpaka ujenzi ukamilike kwa asilimia 100. Shirika limesema kwamba endapo kuna sehemu itakayotumika kabla ya kukamilika kwa asilimia 100, wapangaji watalipa nusu ya kiwango cha kodi.