Saturday, September 16, 2017

MKURUGENZI WA MAENDELEO YA JAMII AONGOZA UCHIMBAJI WA LAMBO KATIKA KIJIJI CHA MANGHANGU, MPWAPWA DODOMA


Sehemu ya vijana wa Kijiji cha Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma wakishiriki kazi ya kuchimba Lambo kwa kutumia nguvu zao wenyewe. 
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akishiriki kuchimbua eneo la Lambo la Kijiji cha Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa Bw. Mohamed Maje akiweka mchanga kwenye ndoo katika zoezi la uchimbaji wa Lambo Kijijini cha Manghungu.
Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Manghungu, kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma wakishiriki kazi ya kuchimba Lambo kwa kutumia nguvu zao wenyewe.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akikabidhi nyundo nzito kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Manghungu, kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw. Sospeter G. Nyaombo kuwezesha kazi ya uchimbaji wa Lambo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akikabidhi jembe kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw. Sospeter G. Nyaombo kuwezesha kazi ya kuchimba Lambo la maji kijijini hapo.
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike akikabidhi chepeo kwa Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw. Sospeter G. Nyaombo wakati wa kushiriki uchimbaji wa lambo kijijini hapo. 
Afisa Mtendaji wa Kijiji cha cha Manghungu, Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma Bw. Sospeter G. Nyaombo akionesha moja ya ndoo zilizotolewa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jmaii, Jinsia Wazee na watoto kuwezesha kazi ya uchimbaji wa Lambo. 
Mratibu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bibi Mwajina Lipinga akijumuika na akinamama kuimba wimbo wa kuhamsha ari ya kuchimba Lambo la maji ya kunywa wakati alipotembelea Kijiji cha Manghungu ,Kata ya Vinghawe Halmashauri ya Mpwapwa mkoani Dodoma.Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Serikali imeadhimia kuwa Sera ya Maendeleo ya Jamii ya mwaka 1996, inatekelezwa kikamilifu na inafuatilia utekelezaji wa Sera hiyo katika ngazi ya mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji mbalimbali hapa nchini.

Akiongea na wananchi wa Kijiji cha Manghangu, kilichoko Kata ya Vinghawe Wilaya ya Mpwapwa mkoani Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jamii Bw. Patrick Golwike amesema Sera hiyo imeweka wazi kuwa wananchi ndiyo kitovu cha maendeleo maana ushiriki wao unatoa dhamana thabiti ya maendeleo na ustawi wa wananchi katika ngazi mbalimbali.

Bw. Patrick Golwike ametanabaisha kuwa lengo la kufika katika Kijiji hicho ni kushirikiana na wananchi kufanya kazi za maendeleo kwa vitendo.

“Kazi ya kuhamsha ari iliyobuniwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inalenga kuhamasisha wananchi kushiriki katika kuibua miradi, kupanga, kutekeleza na kusimamia shughuli za maendeleo kwa kutumia rasilimali zilipo katika mazingira yao ili kujiletea maendeleo yao” alisema Bw. Golwike.

Kwa upande wake Mratibu wa masuala ya Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Rais – TAMISEMI Bibi Mwajina Lipinga, alisema kuwa mradi wa ujenzi wa lambo la maji, na ushiriki wa wananchi katika kazi za kujitolea utakuwa chachu kwa vijana kuhamsha ari ya kujitolea na kuchangia maendeleo ya vijiji na Taifa.

“Kazi hii inayofanyika naomba iwe chachu kwa mikoa mingine ipende kuhamsha ari na kwa kufanya kazi kama kipimo cha heshima na utu wa mtu” alisema Bibi Lipinga.

Aliongeza kuwa, wananchi wanapoona Serikali na wadau wanajitokeza kusaidia kufanya kazi fulani, jamii nayo inawajibu wa kujitokeza katika kushughulikia changamoto zilizopo ili kupata majawabu yenye ufumbuzi wa matatizo hayo kwa manufaa ya wanachi wote.

Akiongea katika zoezi la uchimbaji wa lambo hilo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mpwapwa Bw. Mohamed A. Maje ameahidi kuendeleza kazi ya kushirikiana na jamii katika kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kutumia nguvu za wananchi.

“Nitaandaa matukio mengine mawili ya kuamsha ari ya wananchi kufanya kazi za maendeleo yao ambayo yatasimamiwa na Halmashauri ili kurejesha ushiriki wa wananchi katika kazi za kujitolea” alisema Bw. Maje.

Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Manghangu Bw. Sospeter G. Nyaombo alishukuru Wizara kwa kufika kijijini na kutoa msaada wa vifaa vya uchimbaji wa Lambo pamoja na kushirikiana kazi kwa vitendo.

“Kufika kwenu katika kijiji chetu kumekuwa chachu ya kuchangia maendeleo katika kijiji chetu na maeneo mengine nchini” alisema Bw.Nyaombo.

Vifaa vilivyotolewa na Wizara ni pamoja na majembe 27, chepeo 5, nyundo 3, na ndoo 10.

Mradi wa uchimbaji wa Lambo la maji safi umekadiriwa kukamilika katika kipindi cha siku 15. Chanzo hiki cha maji kitanufaisha kaya zipatazo 538, wananchi 2297, kati yao wanaume wakiwa 983 na wanawake 1314.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...