Saturday, September 09, 2017

SERIKALI ZA TANZANIA NA KENYA ZAMALIZA MZOZO WA VIKWAZO VYA BIASHARA BAINA YA MATAIFA HAYO

Baadhi ya Maafisa Waandimizi wa Serikali, Wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa za Kilimo kutoka wakulima kutoka Tanzania na Kenya wakifuatilia taarifa mbalimbali zilizotolewa na Wenyeviti wa Mkutano huo uliojadili changamoto na utatuzi wa vikwazo vya biashara na uwekezaji katika Mataifa hayo.
Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dkt. Pindi Chana akitoa taarifa ya majadiliano ya mkutano baina ya Watendaji Wakuu wa Serikali ya Tanzania na Kenya uliojadili changamoto na utatuzi wa vikwazo vya biashara na uwekezaji katika Mataifa. Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam. Wengine katika Picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Tanzania, Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Kenya Dkt. Chris Kiptoo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji (Baishara na Uwekezaji), Prof. Adolf Mkenda akizungumza na Watendaji Wakuu wa Serikali, Wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa za kilimo katika Mataifa hayo. Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam. Wengine katika Picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Tanzania, Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Kenya Dkt. Chris Kiptoo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Ushirikiano wa Kenya, Dkt. Chris Kiptoo akizungumza na Watendaji Wakuu wa Serikali, Wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa za kilimo katika Mataifa hayo. Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam. Wengine katika Picha ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Tanzania, Prof. Adolf Mkenda na Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara ya Kenya Dkt. Chris Kiptoo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara, Uwekezaji na Ushirikiano wa Kenya, Dkt. Chris Kiptoo na Mwenjeji wake Prof. Adolf Mkenda wakionyesha Sera ya Taifa ya Biashara ya Kenya wakati mkutano baina ya Watendaji Wakuu wa Serikali, Wafanyabiashara na Wazalishaji wa bidhaa za kilimo katika Mataifa hayo uliojadili changamoto na utatuzi wa vikwazo vya biashara na uwekezaji katika Mataifa hayo. Mkutano huo ulifanyika jana Septemba 8 Jijini Dar es Salaam.(PICHA NA ELIPHACE MARWA-MAELEZO)

Na Ismail Ngayonga-MAELEZO-DAR ES SALAAM

SERIKALI za Tanzania na Kenya zimekubaliana kwa pamoja kumaliza vikwazo vya kibiashara katika usafirishaji na uingizaji wa bidhaa katika mipaka baina ya nchi hizo mbili hatua inayokusudia kuimarisha ushirikiano wa biashara na uwekezaji katika Mataifa hayo.

Hayo yamesemwa jana Jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Wizara, Biashara na Uwekezaji (Biashara na Uwekezaji) Prof. Adolf Mkenda mara baaada ya kumalizika kwa mkutano wa pamoja yao ulioshirikisha Viongozi Waandamizi wa Serikali hizo, Wafanyabiashara na Wakulima kutoka Mataifa hayo.

Anasema katika mkutano huo Serikali ya Tanzania iliwasilisha mapendekezo 15 kwa Serikali ya Kenya yanayopaswa kupatiwa ufumbuzi, ambapo kwa upande wa Kenya waliwasilisha mapendekezo 16 ambapo kwa kiasi kikubwa hoja hizo zimekubaliwa na kupatiwa majibu yake katika mkutano huo.

Prof. Mkenda alisema kupatikana kwa mwafaka wa majadiliano hayo ni maelekezo ya Viongozi Wakuu wa Mataifa hayo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa Tanzania na Uhurru Kenyatta wa Kenya kwa kuwa Viongozi hao wametaka suala hilo lipatiwe mwafaka wa haraka ili kuweza kuendeleza ushirikiano na uhusiano katika nyanja mbalimbali baina ya nchi hizo.

Kwa mujibu wa Prof. Mkenda alisema mkutano huo uliofanyika kwa muda wa siku tatu ulilenga kumaliza changamoto za biashara zinazojitokeza kwa Wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya, ambapo Timu za Wataalam wa Serikali hizo ambapo hoja hizo zimeweza kujadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wa pamoja, hatua inayolenga kufungua upya milango ya ushiriakiano baina ya Wafanyabiashara na Wakulima wa Tanzania na Kenya. 

“Katika majadiliano yetu tumekubaliana kuwa sasa bidhaa ya gesi ya kupikia na ungano wa ngano ambazo zilizuliwa kuingia Kenya sasa zitaruhusiwa kuingia nchini humo, na sisi kwa upande wetu Tanzania tumeruhusu maziwa na sigara kutoka Kenya zianze kuingia nchini” alisema Prof. Mkenda.

Akifafanua zaidi Mkenda anasema Mkutano huo pia uliwashirikisha Wafanyabiashara na Kampuni za uzalishaji wa bidhaa za ngano ikiwemo kampuni ya Azam Bakhressa ambayo huzalisha na kusambaza ngano hapa nchini pamoja na nchi jirani ikiwemo Kenya pamoja na wakulima wa zao hilo kutoka mikoa ya Sumbawanga, Iringa na Manyara.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Ushirikiano ya Kenya, Dkt. Chris Kiptoo alisema Serikali ya Kenya itayachulia kwa uzito unaostahili mwafaka wa majadiliano hayo, kwa kuzingatia kuwa Serikali ya Tanzania na Kenya zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu katika masuala ya biashara na uwekezaji.

Alisema kuwa Serikali ya Kenya imewekeza jumla Dola Bilioni 1.5 katika sekta ya viwanda, ambapo hadi sasa vimeweza kuajiri jumla ya watu 50,000 na pia msingi wa biashara ya Kenya katika Tanzania imeweza kuongeza kutoka Tsh. Bilioni 17 mwaka 2004 hadi kufikia Dola Bilioni 34 mwaka 2015.

Dkt. Kiptoo anasema mara baada ya mkutano huo, Viongozi wa Serikali hizo pamoja na Wafanyabiashara kutoka upande za Tanzania na Kenya wanatarajia kukutana kwa mara ya mwisho Mombasa nchini Kenya kwa ajili ya kuhitimisha makubaliano ya pamoja ya uingizaji na usafirishaji wa bidhaa.

Akifafanua zaidi Dkt. Kiptoo anasema katika majadiliano hayo Idara muhimu zinazohusika na masuala ya biashara na uwekezaji kutoka Serikali za Tanzania na Kenya zilishiriki katika mkutano huo, ikiwemo Maafisa wa Idara za forodha, kodi na ushuru.

Tarehe 3 Agosti mwaka huu, Viongozi Waandamizi wa Serikali za Tanzania na Kenya walikutana katika Mpaka wa Namanga kwa ajili ya kikao cha majadiliano ya pamoja kilicholenga kumaliza mzozo wa kuzuiwa kwa Wafanyabiashara ya Ngano nchini kuingiza bidhaa hiyo nchini Kenya.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...