Thursday, September 28, 2017

MARUFUKU SHULE MKOANI SINGIDA KUNUNUA CHAKI NJE YA MKOA-RC NCHIMBI

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akishiriki zoezi la kutengeneza chaki katika kiwanda cha Dober Color Kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Mkuu wa Wilaya ya Manyoni Miraji Jumanne Mtaturu akiwa amebeba ili kuzianika chaki alizotengeneza Mkoa Singida Dkt Rehema Nchimbi katika kiwanda cha Dober Color Kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikagua kiwanda cha kutengeneza jasi cha Dober Color Kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi.
Wafanyakazi wa kiwanda cha Dober Color wakifungasha chaki, Meneja wa Kiwanda hicho amesema sehemu ya kufungasha chaki hiyo inafanywa na wanawake kwakuwa wako makini na haraka.
Mkuu wa Mkoa Singida Dkt Rehema Nchimbi akikagua ubora wa chaki inayozalishwa katika kiwanda cha Dober Color Kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Itigi, kushoto kwake ni Meneja wa Kiwanda hicho Abdul Razak Mahamoud.


Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amepiga marufuku Shule zote Mkoani Singida kuagiza chaki nje ya Mkoa kwakuwa kuna viwanda vinavyozalisha chaki bora mkoani hapa.

Dkt Nchimbi ametoa katazo hilo mara baara ya kufanya ziara katika viwanda viwili vinavyozalisha chaki katika halmashauri ya Itigi na kushuhudia chaki yenye ubora ikiwa imezalishwa kwa wingi na ikiwa haijapata soko.

“Hawa wenye viwanda wamejitahidi kuzalisha chaki bora haina vumbi na inauzwa kwa bei sahihi lakini shule zetu badala ya kuja kununua hapa ambapo ni karibu wanaagiza Dar es salaam na mikoa mingine”, amesema na kuongeza kuwa,

“Yani mnasubiri chaki hii hii iende Dar es Salaam halafu mnainunulia kutoka huko, hii haikubaliki, kuanzia leo shule zote zinunue chaki hapa hapa ili tupunguze gharama pamoja na kuinua viwanda vyetu”.Dkt Nchimbi ameongeza kuwa Mikoa ya Jirani itakayonunua chaki katika Viwanda vya Singida, vitasafirishiwa chaki hiyo bure kama motisha kwa kuunga mkono viwanda hivyo.

Amezitaka halmashauri kushirikiana katika kuboresha mazingira ya utendaji wa viwanda hivyo hasa kwa kuangalia namna ya kuboresha barabara zinazoenda katika machimbo ya jasi yanayotumika kutengeneza chaki kwakuwa wenye viwanda wamekuwa wakilalamikia ubovu wa barabara hizo.

Aidha Dkt Nchimbi ametoa wito kwa wenye viwanda wote nchini ambao wanatumia madini ya jasi (gypsum) katika shughuli zao wasihangaike kutafuta madini hayo bali waje singida kuna viwanda vinatengeneza madini hayo kwa ubora mzuri na bei nzuri.

Amesema viwanda vya kutengeneza jasi Singida vimekuwa vikizalisha madini hayo kwa wingi hivyo wenye uhitaji wa madini hayo kutengenezea chaki, gypusum board POP, wanakaribishwa kununua madini hayo mkoani hapa.

Dkt Nchimbi amewapongeza wenye viwanda hivyo kwa kutumia rasilimali kama madini ya jasi iliyopo Singida kwa kuanzisha viwanda mabavyo vinatengeneza ajira na kukuza uchumi kwa kuwa wao wamekuwa walipa kodi wazuri.

Naye Meneja wa kiwanda cha chaki cha Dober Color kilichopo Itigi Abdul Mahamoud amemshukuru Mkuu wa Mkoa kwa hatua yake ya kukataza kuagizwa chaki nje ya Singida kwakuwa kutaongeza soko ambalo litasaidia viwanda hivyo kukua.

“Mkuu wa Mkoa tunashukuru kwa katazo hilo kwakuwa litafanya viwanda vyetu vikue na kuongeza uzalishaji, lakini pia itafanya viwanda hivi viongeze ajira na hata kodi tunayolipa itaongezeka hivyo kukuza uchumi wa Singida”, amesema Mahamoud.

Ameongeza kuwa kwa sasa kiwanda hicho kinazalisha tani hamsini kwa siku lakini kutokana na katazo hilo matarajio ni kuongezeka uzalisha hadi kufikia tani 200 za chaki kwa siku.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...