Friday, December 20, 2024

WANANCHI 96 KUTOKA ENEO LA HIFADHI YA NGORONGORO WAPOKELEWA NA KUKABIDHIWA MAKAZI YAO MSOMERA





Na Mwandishi Wetu, Handeni, Tanga 

Jumla ya kaya 22 zenye watu 96 na mifugo 196 zilizokubali kuhama kwa hiari kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro zimepokelewa rasmi katika Kijiji Msomera, Wilayani Handeni na kukabidhiwa makazi yao leo Disemba, 19 2024. 

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Handeni Albert Msando, Katibu tarafa wa tarafa ya Sindeni Bw. Baraka Nkatura alisema kwamba Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kwamba wananchi hao waliokubali kuhama kwa Hiyari wanapatiwa huduma bora kama walivyoahidiwa. 

“Baada ya kupokelewa nipende kuwahakikishia kuwa Serikali imejipanga vizuri na vitu ambavyo mliahidiwa  kuwa matavikuta Msomera viko tayari. Mtapatiwa nyumba iliyojengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa hekari 2.5, Shamba la Ekari 5, Pamoja na maeneo yaliyotengwa mahususi kwa ajili ya shughuli za ufugaji” Alisema Baraka

Baada ya kukabidhiwa nyumba, Bw. Samweli Koromo ambaye ni mmoja wa wananchi waliopokelewa Msomera Alisema kuwa wamefurahi sana baada ya kuona kwamba  wana uwezo wa kumiliki nyumba za kisasa tofauti na ilivyokuwa huko Hifadhini ambako sheria za uhifadhi zilikuwa haziruhusu kufanya ujenzi wa makazi bora ya kudumu. 

“Nimefurahi sana nimepata Nyumba nzuri kwani kule Ngorongoro tulikuwa hatuwezi kujenga wala kufanya shughuli za maendeleo, na pia tumefika msimu wa mvua hivyo nitaanza kufanya maandalizi kwa ajili ya kilimo” Alisema Samwel 

Kwa upande wake Bi. Esther Naftal ambaye kwa sasa ni mkazi wa Msomera akitokea Ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro takriban miaka mitatu iyopita, alisema kwamba wanafarijika kuona ndugu zao wanaendelea kupata mwitikio wa kujiandikisha na kuhama kwa hiari kuja Msomera.

“Sisi tuliokuja mwazoni tumeshaona mazuri ya Msomera kwa sasa tuna chakula cha kutosha baada ya kulima, tumeanzisha biashara, Watoto wetu wanasoma shule, kwa ujumla maisha yetu yamekuwa bora zaidi. Wito wangu kwa ndugu zetu waliobaki Ngorongoro wajiandikishe ili waweze kunufaika na furasa hii tuliyopewa na Serikali” Alisema Esther

Serikali kupitia Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na zoezi la utoaji Elimu, uandikishaji na uhamishaji wa wananchi wanaohama kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kwa hiari kuelekea Msomera na maeneo mengine waliyochagua wenyewe.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...