Na Philomea Mbirika, NCAA.
Jumla ya wananchi 97 waliokubali kuhama kwa hiari kutoka ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro Kwenda Kijiji cha Msomera wilaya ya Handeni Tanga, wametoa wito kwa wananchi wenzao waliobaki ndani ya hifadhi kujiandikisha ili wapate uhuru na fursa ya kuboresha maisha yao nje ya Hifadhi na kuepuka hatari ya kuishi na wanyama wakali katika eneo moja.
Wito huo umetolewa leo tarehe 19 Desemba 2024 na wawakilishi wa wananchi hao ambapo kundi la 21 la awamu ya pili lenye kaya 23, watu 97 na mifugo 196 limehama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro kuelekea Kijiji cha Msomera na maeneo Mengine waliyochagua wenyewe.
Bw. Daudi Melubo kutoka kijiji cha Kayapus ambaye ni mmoja wa wananchi waliohama leo amesema yeye na familia yake waliamua kufanya maamuzi ya kuhama ndani ya Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro kutokana na kutokua na uhuru wa kujiendeleza kiuchumi kutokana na sheria za uhifadhi.
“Mimi nimeamua kuhama kwa hiyari yangu kwenda Msomera kwa sababu huko kuna uhuru wa kujiendeleza, nitajenga nyumba, nitamiliki ardhi, watoto wangu wataenda shule bila hofu ya mnyama na hakuna sheria kama hifadhini, nawashauri ndugu zangu ambao bado hawajajiandikisha kuhama kwa hiari na watapata fursa ya kuendeleza na kuboresha maisha yao” Alisema Daudi
Kwa upande wake, Bi. Naishiye Sembeta alieleza kuwa;
“Sisi wanawake tumekuwa tukitembea umbali mrefu kwenda kutafuta kuni porini huku tukihatarisha maisha yetu, ila sasa tunahamia Msomera na tunaamini maisha yetu yatabadilika na kuwa bora zaidi” alisema Naishiye
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa zoezi hilo, Meneja wa mradi Afisa uhifadhi Mkuu Flora Asey amesema kuwa hadi kufikia leo tarehe 19/12/2024 jumla ya kaya 1,678 zenye watu 10,073 na mifugo 40,593 zimekwisha hama ndani ya Hifadhi kuelekea Msomera na wengine kwenye maeneo waliyochaguwa wenyewe.
Assey alisisitiza kuwa kwa sasa utaratibu uliopo ni kuhakikisha kuwa zoezi la uandikishaji, tathmini ya maendelezo na uhamishaji vinaenda sambamba ili kuhakikisha kila mwananchi anapojiandikisha anatumia muda mfupi kuhama ndani ya hifadhi kwenda eneo alilochagua
Zoezi la kuhama kwa hiari ndani ya hifadhi ya Ngorongoro linaendelea ambapo adhma ya Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha kuwa wananchi hao wanapata fursa ya kuishi katika maeneo salama yenye huduma zote muhimu za kijamii kwa ajili ya maendelea ya wananchi hao.
No comments:
Post a Comment