Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa (Mb) ameiagiza Menejimenti ya Wizara ya Mambo ya Ndani kusimamia Kitengo kinachoshughulikia Malalamiko yanayotolewa kwa Wizara, Taasisi na Vyombo vya Usalama kuhakikisha wanayafanyia kazi na kutoa mrejesho wa utatuzi wa malalamiko kwa Wananchi.
Aidha, Bashungwa amevitaka Vitengo vya Mawasiliano na Habari vya Wizara, Vyombo vya Usalama na Taasisi zote kuboresha mfumo wa Mawasiliano na habari kwa umma.
Ameeleza hayo leo tarehe 12 Disemba, 2024 wakati akizungumza na Wakuu wa Idara na Vitengo mara baada ya kupokelewa Makao Makuu ya Wizara yaliyopo Mji wa Serikali Mtumba – Dodoma na kusisitiza kuwa ni haki ya Watanzania kupata taarifa sahihi kwa wakati.
“Kuna Malalamiko mengine yanakuwepo kwa sababu hamna taarifa sahihi au taarifa imechelewa, kwahiyo lazima mhakikishe mnashughulikia Malalamiko na kutoa mrejesho”, ameeleza Bashungwa.
Vilevile, Bashungwa ametoa wito kwa Watumishi wa Wizara kutoa ushirikiano kwake na viongozi wengine wote ili kwa pamoja kutimiza adhima ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwahudumia Wananchi.
No comments:
Post a Comment