Dkt. Samia, Mvumbuzi Zinjanthropus Boisei Dkt. Leakey Kutuzwa Tuzo za Utalii na Uhifadhi 2024





Mambo yanaiva zaidi katika sekta ya utalii na uhifadhi nchini ambapo Disemba 20 mwaka huu dunia itashuhudia uzinduzi wa Tuzo za Utalii na Uhifadhi, za kwanza kitaifa Tanzania, ambapo viongozi na watu mashuhuri wenye mchango katika sekta hizo watatuzwa mwaka huu na baadaye kila mwaka. 

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha leo Disemba 18, 2024, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi amesema licha ya kuzindua lakini tuzo chache za heshima na shukrani zitatolewa ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na mvumbuzi wa fuvu la mwanadamu wa kale (Zinjanthropus Boisie), Dkt. Louis Leakey na mkewe Mary Leakey ambaye baadaye naye na watafiti wenzake walivumbua pia nyayo za binadamu wa kale aliyetembea akiwa wima (Laitori) watakuwa miongoni mwa watakaopewa Tuzo za heshima. 

“Tutazindua na tuzo 11 za heshima na shukrani na ya kwanza itaenda kwa Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mwanamaono mkuu ambaye mchango wake kupitia filamu ya Royal Tour na baadaye Amazing Tanzania umekuwa limbuko katika sekta ya utalii na uhifadhi. 

“Dkt. Leakey na familia yake watatuzwa pia kama moja ya kutambua watu ambao matendo yao, ubunifu na tafiti zao zimetuzalishia vivutio muhimu vya utalii wetu wa sasa. Leo kwa mwaka pale Olduvai wanafika wastani wa watalii 20,000 hawa leo hawako hai lakini kazi ya mikono yao inaendelea kuleta matokeo chanya. Hivi ndivyo namna tutakavyotambua wadau wengi zaidi kila mwaka kuenzi mchango wao,” alisema Dkt. Abbasi.

Katika tukio hilo Mgeni Rasmi atakuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisindikizwa na Waziri wa Sekta, Dkt. Pindi Chana na Naibu Waziri Dunstan Kitandula, mawaziri, wakuu wa mikoa, makatibu wakuu na wadau wa utalii ndani na nje ya nchi.

Aidha, kutakuwa na burudani mbalimbali kutoka kwa wasanii kama kundi la Weusi, Frida Amani, Sholo Mwamba na vikundi kutoka mataifa ya India na China kuupamba usiku huo. 

Tuzo hizo zitakuwa zikitolewa kila mwaka kuenzi mchango wa wadau wa ndani na nje ya nchi katika sekta hizo zinazoongoza kwa sasa nchini kuliletea Taifa fedha za kigeni.

Comments