Zanzibar, Desemba 26, 2024 — Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuonyesha upendo na kujali watu wenye mahitaji maalum nchini.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi za Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya kwa niaba ya Rais Samia katika Makazi ya Wazee Zanzibar, Mhe. Mwanaidi amesema kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum, hususan watoto na wazee, wanapatiwa huduma muhimu na mazingira bora ya kuishi.
"Mheshimiwa Rais ni kiongozi mwenye huruma na upendo kwa wananchi wote. Inapofika msimu wa sikukuu, ni kawaida yake kutoa zawadi kwa watoto, wazee, na wananchi wengine ili kuhakikisha wanafurahia kwa pamoja. Leo ameona ni vema kuwafikia wananchi wa Zanzibar," alisema Mhe. Mwanaidi.
Naibu Waziri aliwataka wananchi kote nchini kutumia msimu huu wa sikukuu kwa kuonyesha upendo na mshikamano kwa wenye mahitaji maalum kwa kuwasaidia mahitaji ya msingi na kuwapa faraja.
Alimalizia kwa kuhimiza jamii kushiriki kwa vitendo katika kuwajali wazee, watoto, na makundi maalum kwa ujumla, hasa wakati huu wa sherehe za mwisho wa mwaka.
Zoezi hilo limeleta tabasamu na faraja kwa wazee walioko katika makazi hayo, huku wakimshukuru Rais Samia kwa moyo wa huruma na mshikamano anaouonyesha mara kwa mara.
Comments