Tuesday, December 31, 2024

Benki ya CRDB yafungua matawi mapya Mugango, Sirari mkoani Mara

 

Katika kuufunga mwaka 2024 kwa huduma bora, Benki ya CRDB imefungua matawi mapya mawili mkoani Mara yaliyopo Mugango katika Wilaya ya Musoma Vijijini na Sirari wilayani Tarime. 

Afisa Mkuu wa Biashara wa Benki ya CRDB, Boma Raballa amesema uzinduzi wa matawi hayo ni sehemu ya jitihada za Benki kuiishi kaulimbiu yake ya ‘ulipo, tupo’ kwa kuwafuata wananchi katika kila pembe ya nchi na kuwapa huduma bora za fedha kwa maendeleo yao binafsi na kuchangia uchumi wa taifa pia. 
 “Mkoa wa Mara una shughuli nyingi za kiuchumi kuanzia migodi mikubwa na machimbo ya madini, uvuvi, kilimo na biashara ya mpakani hivyo ni muhimu kuwa na huduma za uhakika za fedha ili kuwajumuisha wananchi kwengi katika uchumi. Ulikuwa ni mpango wa Benki yetu ya CRDB kuhakikisha tunafungua matawi haya mawili kabla mwaka 2024 haujaisha,” anasema Raballa. 


Kabla ya ufunguzi wa matawi hayo mapya, Raballa amesema wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata huduma za benki kupitia kwa mawakala waliotapakaa maeneo tofauti. Kwa mkoa mzima wa Mara, amesema Benki ya CRDB inao zaidi ya mawakala 600 wakiwamo 195 wanaohudumia katika Wilaya Ya Tarime na 35 Musoma Vijijini. 
 

“Kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya wateja wilayani Tarime na Musoma, Benki yetu iliona kuna umuhimu wa kuboresha huduma ili kuendana na mahitaji yaliyopo sasa na yatakayojitokeza baadaye. Tulifanya utafiti wa kina kabla ya kujenga matawi haya yatakayowahudumia wananchi wa Mugango na Sirari pamoja na maeneo jirani,” amesema Raballa. 

Kutokana na uzinduzi wa matawi hayo mawili, Benki ya CRDB sasa imefikisha jumla ya matawi 10 mkoani Mara ambayo ni Musoma, Tarime, Bunda, Serengeti, Nyamongo, Rorya, Shirati, Mugango na Sirari hivyo kuifanya kuwa na mtandao mpana zaidi wa matawi nchini kuliko benki nyingine yoyote nchini.
 

Akifungua tawi la Sirari, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Mheshimiwa Meja Edward Flowin Gowele amesema huduma za fedha ndio msingi wa maendeleo ya mwananchi binafsi, kaya na taifa kwa ujumla hivyo kilichobaki ni umakini wa wananchi kubuni miradi itakayowainua kiuchumi kwa kuzikabili changamoto zilizopo kwenye maeneo yao ili kunufaika na fursa zinazojitokeza.

“Tawi hili ni sehemu salama kwa wananchi kuhifadhi akiba zenu za fedha. Ni mahali ambapo wafanyabiashara mtapata mikopo ya kuimarisha miradi yenu na wafanyakazi nao wataweza kutimiza malengo yao. Benki ni rafiki wa kila mwananchi anayewa na kupanga maendeleo yake, tulitumie tawi hili kujinufaisha kwa kujenga uchumi imara wa kila mmoja wetu,” amesema Mheshimiwa Gowele. 

Licha ya kunufaika na mikopo inayotolewa, Mheshimiwa Gowele amewahimiza wananchi wa Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara na Tanzania nzima kwa ujumla kuwekeza kwenye Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond inayoendelea kuuzwa na Benki ya CRDB ili kupata fedha zitakazowezesha ujenzi wa barabara zilizo chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA). 
 

“Ukiwekeza katika hatifungani hii una uhakika wa kupata faida ya asilimia 12 inayotolewa kila mwaka kwa muda wote wa miaka mitano wa uhai wake. Lakini, kumiliki hatifungani hii ni sawa na kuwa na nyumba, unaweza kuitumia kama dhamana kuchukua mkopo kutoka taasisi yoyote ya fedha. Nawasihi kila mmoja wenu na Watanzania wote kwa ujumla, kuitumia fursa hii kuwekeza kwenye hatifungani hii,” amesisitiza Mheshimiwa Gowele. 

Kwenye uzinduzi wa tawi la Mugango, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Musabila Kusaya amesema ni fursa kwa wananchi wa Musoma kunufaika na huduma zinazotolewa na Benki ya CRDB zikiwamo zilizo chini ya Programu ya Imbeju inayolenga kuwawezesha vijana na wanawake. 
 

“Ufunguzi wa tawi hili umesogeza kwa karibu fursa za Programu ya Imbeju. Nawaomba wajasiriamali mlitumie tawi hili kupata mitaji wezeshi itakayosaidia kuinua biashara zenu. Hapa, mtapata ushauri wa kitaalamu ia wa namna bora ya kukuza shughuli zenu kwa maendeleo binafsi na taifa pia,” amesema Kusaya. 

Sambamba na ufunguzi wa tawi la Benki ya CRDB Sirari, Benki ya CRDB imekabidhi madawati 50 yenye thamani ya shilingi milioni 5 kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzi kwa wanafunzi wa Wilaya ya Tarime. Madawati hayo yamepokelewa na Mheshimiwa Gowele aliyesema yatasaidia kupunguza uhaba uliopo katika shule za msingi na sekondai wilayani Tarime. 

Monday, December 30, 2024

RAIS DKT. SAMIA AMLILIA MAREHEMU MHESHIMIWA JAJI MWANAISHA KWARIKO

 






-Asema alikuwa alikuwa ni moja ya majaji wa mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa

WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa leo Desemba 30, 2024 amemwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.

Akitoa Salama pole kwa waombolezaji nyumbani kwa marehemu Kondoa, Mkoani Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Rais Dkt. Samia ameguswa na kifo cha Mheshimiwa Mwanaisha kwani alikuwa ni moja ya majaji wa mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa katika nafasi zote alizozitumikia.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Marehemu Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa kiongozi aliyetekeleza wajibu wake kwa weledi na uadilifu “Msiba huu kwetu ni mzito, jukumu letu Wanakondoa, Watanzania, Majaji na wajumbe wa Tume ni kuendelea kumuombea kwa Mwenyezi Mungu”

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kila mmoja kuenzi yote mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Mwanaisha katika kipindi chake chote cha utumishi wa umma kwani kufanya hivyo kutakuwa ni njia nzuri ya kuweka kumbukumbu ya kazi zake.

Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko aliishi kiapo cha Uhakimu kwa kutoa huduma kwa wananchi ikiwemo kutatua migogoro kwa uadilifu bila upendeo wowote,

“Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa na ubinadamu na utu, maisha yake yalikuwa ni yakusaidia watu wengine, sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani uhai wake umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kimahakama”

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji (Rufani) Jacobs Mwambegele amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha ameondoka katika kipindi ambacho tume ilikuwa inamuhitaji hasa katika kipindi hiki ambacho tume hiyo ipo katika mchakato wa kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani

“Tumempoteza Mheshimwa Mwanaisha tukiwa kwenye mzunguko wa nane wa zoezi la kuboresha daftari na tukiwa tunaingia kwenye mzunguko wa tisa utakaohusiaha mikoa minne Rukwa, Songwe, Njombe na Ruvuma, pia mara zote alitoa ushauri wenye weledi wa hali ya juu katika kuhakikisha tume inatekekeza majukumu yake kwa kuzingatia katiba sheria kanuni na taratibu”.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa ni kiongozi mwenye msimamo na mtetezi wa masuala ya wanawake, “alibobea katika eneo ambalo alikuwa anafanyia kazi, sisi wanadodoma tutamkumbuka kwa machango wake mkubwa kwenye masuala ya maendeleo”

Marehemu Mheshimiwa Jaji wa Mahakama ya Rufani Mwanaisha Kwariko alifariki Desemba 27, 2024 nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.

Sunday, December 29, 2024

Dkt. Yahaya Nawanda: Imani kwa Mungu Yamenisaidia Kushinda Changamoto za Maisha


Aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Dkt. Yahaya Nawanda, amesema kuwa imani yake kwa Mungu imemsaidia kuvuka kipindi kigumu maishani mwake.

Akizungumza jana kwenye misa ya kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan na kumkumbuka baba mzazi wa Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa, iliyofanyika Nyakabindi, Bariadi, Dkt. Nawanda alieleza kuwa changamoto za maisha ni mitihani ya imani na uvumilivu.

“Nimepitia kipindi kigumu sana, lakini Mungu humpatia mtu mtihani ambao anajua anaweza kuushinda. Leo, kwa nguvu za Mungu, naweza kusema nimefanikiwa kushinda,” alisema Dkt. Nawanda.

Katika hotuba yake, aliongeza kuwa kesi iliyokuwa ikimkabili ilimfundisha thamani ya kuishi kwa amani na kushirikiana na watu. Alitoa shukrani za pekee kwa wananchi wa Simiyu kwa mapenzi na maombi yao yaliyompa nguvu wakati wa changamoto hiyo.

Ikumbukwe kuwa mnamo Novemba 20, 2024, Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Simiyu ilimwachia huru Dkt. Nawanda baada ya kutomkuta na hatia katika kesi ya kulawiti iliyokuwa inamkabili.

Dkt. Nawanda alihitimisha kwa kusisitiza umuhimu wa kumtumainia Mungu na msaada wa jamii katika kushinda changamoto za maisha, akiwataka watu wote waendelee kuwa na imani na mshikamano.


Churchill Show Tanzania yafana Arusha













Wakali wa kuvunja mbavu toka Tanzania na Kenya wakutana ndani ya ‘Churchill Show Tanzania’ jijini Arusha usiku wa Desemba 28, ikiwa ni utangulizi tu wa sherehe za kuuaga mwaka 2024 na kuukaribisha mwaka 2025 katikati ya Arusha kuanzia tarehe 29 Desemba, 2024 hadi 1 Januari, 2025 zilizoandaliwa na uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.

Wakijumuika pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda usiku wa leo ni pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mhe. Felician Mtahengerwa,  Balozi wa Kenya nchini Tanzania, Mhe. Isaac Njenga, Balozi wa Somalia nchini Tanzania, Mhe. Ilyas Ali Hassan pamoja, Mchungaji Tony Osborn kati ya viongozi na watu wengine mashuhuri. 

Burudani hiyo ya vichekesho imewajumuisha wachekeshaji maarufu kutoka Kenya na Tanzania akiwemo Eliud Samwel, Churchill, Chipukeezy, Mzee Shayo na Eric Omondi.

Saturday, December 28, 2024

Mil. 76/- kati ya Mil. 300/- za NMB MastaBata zaenda kwa wateja 712

 


NA MWANDISHI WETU

WATEJA zaidi ya 700 kati ya 2000 wa msimu wa sita wa promosheni ya kuhamasisha malipo na manunuzi kwa njia ya kadi inayoendeshwa na Benki ya NMB ‘NMB MastaBata – La Kibabe,’ wameshajizolea kitita cha jumla cha zaidi ya Sh. Mil. 76.4, kati ya zaidi ya Mil. 300 zinazoshindaniwa kupitia droo za kila wiki.

NMB MastaBata – La Kibabe ni kampeni inayochagiza matumizi yasiyo ya pesa taslimu, ambako wateja wa NMB wanaotumia Kadi za MastaCard kuchanja kulipia huduma kwa njia ya QR Code, PoS na NMB Pay by Link, ambapo benki hiyo huwazawadia kila wiki, kila mwezi na ‘grand final’ itakayofanyika Februari 12, 2025.

Idadi hiyo ya washindi na kiasi hicho cha pesa walizoshinda, kimekuja baada ya kufanyika kwa droo ya saba, iliyofanyika Ijumaa Desemba 27, kwenye Ofisi za NMB Tawi la Tegeta, ambako Meneja wa Tawi, Bi. Magreth Lwiva, alichezesha akisimamiwa na Pendo Mfuru kutoka Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT).

Akizungumza kabla ya droo hiyo, Bi. Magreth alisema jumla ya washindi 2000 watajishindia zawadi mbalimbali zilizotengwa na benki hiyo zikiwa na thamani ya Sh. Mil. 300 na kwamba kila wiki wateja 100 hujinyakulia kiasi cha Sh. 100,000, huku wengine 40 wakishinda zawadi za papo hapo, zikiwemo vocha za manunuzi ‘shopping challenge.’

“NMB MastaBata pia hutoa zawadi za kila mwisho wa mwezi kwa miezi miwili, ambako washindi 15 hujinyakulia Sh. 500,00 kila mmoja, washindi watano hujishindia safari ya kutembelea Mguga za Wanyama za Mikumi na Ngorongoro na wengine watano kujishindia pesa hadi Sh. Mil. 4 za ada zao au watoto wao.

“Katika droo ya mwisho yaani grand finale, wateja wetu sita watajishindia tiketi za kusafiri Kwenda Dubai wao na weza wao, ambapo wataka huko kwa siku tano kwenye Hoteli ya Nyota Tano, safari ambayo itagharamiwa kila kitu na NMB,” alibainisha Bi. Magreth mbele ya Afisa wa Idara ya Biashara ya Kadi NMB, Salehe Nkuruvi.

Kwa upande wake, Bi. Pendo Mfuru kutoka GBT, alisema Bodi yake inaishukuru NMB kwa namna inavyoendesha droo zake kwa uwazi na haki, huku akiwataka wateja wa benki hiyo kuwa huru wanaposhiriki droo mbalimbali, kwani inazingatia sheria, kanuni na miongozi wanayopewa na GBT.

“Niko hapa kwa niaba ya GBT, uwepo wangu hapa unalenga kuhakikisha droo inachezeshwa kwa kuzingatia vigezo na masharti yanayosimamia michezo hii, ili kupata wateja kihalali, ambalo ndilo jukumu mama la taasisi yetu. Hivyo tunawahakikishia wateja wa NMB kwamba, haki, vigezo na masharti vinazingatiwa,” alisema.











TASHICO YAFAFANUA MELI MV SERENGETI KUZAMA ZIWA VICTORIA




 NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA

KAMPUNI ya Meli Tanzania (TASHICO) imefafanua tukio la kuzama kwa meli ya MV Serengeti katika Bandari ya Mwanza Kusini,Ziwa Victoria, baadaa ya kukumbwa na tatizo la kuegemea upande wa nyuma na kutitia chini ndani ya maji.

Akizungumza na waandishi wa Habari, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TASHICO, Wakili Alphonce Paul Sebukoto, ameeleza kuwa tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Disemba 26, majira ya saa 8:00 usiku, ambapo meli ilionekana kulalia upande wa nyuma na kuzama majini.

Amesema kuwa walipokea taarifa ya meli hiyo kuingiza maji na hivyo kuzama upande wa nyuma baada ya kuelemewa na maji , ikiwa imeegeshwa katika ghati eneo la Bandari ya Mwanza Kusini, wilayani Nyamagana.

“Meli haijafanya biashara muda mrefu ilikuwa imeegeshwa tangu mwaka 2016, ikisubiri kufanyiwa ukarabati mkubwa. Hii ni meli ambayo ilisitisha kutoa huduma ya usafirishaji wa mizigo na abiria,” amesema Wakili Sebukoto.

Amesema MV Serengeti, imetengewa fedha za ukarabati ni moja ya meli nne zilizokuwa zimesimamishwa na serikali ili kufanyiwa ukarabati mkubwa,zingine ni MT Ukerewe, MV Nyangumi na ML Wimba na zinakaguliwa kila mwaka na wataalamu wa kiusalama ili kuhakikisha usalama wa meli hizo.

“MV Serengeti haikuwa na matatizo yoyote ya kiusalama,iko katika mpango wa matengenezo mwaka huu wa fedha 2024/25.Meli hii inakaguliwa kila mwaka na wataalamu wa usalama na siku chache kabla ilikaguliwa na kuonekana iko salama.”

Wakili Sebukoto ameongeza kuwa chanzo cha meli hiyo kujaa maji bado hakijajulikana, na kuna uwezekano wa kuchakaa kwa baadhi ya vyuma vya meli, au kupigwa mawimbi makali ambayo yanaweza kuleta tatizo hilo.

Amesema bado ni mapema kusema nini kimesababisha meli ilemewe na maji hadi kuzama upande wa nyuma, hivyo baada ya kunyayuliwa utafanyika uchuguzi wa kitaalamu kuibaini tatizo.

“Meli hii iliyojengwa mwaka 1988 ina uwezo wa kubeba abiria 500 na tani 250 za mizigo. Ni meli muhimu yenye faida kwa TASHICO na serikali, hasa katika maeneo yasiyo na miundombinu ya bandari, ikiwemo visiwani,” amesema Wakili Sebukoto, akisisitiza umuhimu wa ukarabati wa meli hiyo.

Akijibu maswali kuhusu tukio lingine la meli ya MV Clarias, Wakili Sebukoto amefafanua kuwa, hilo halihusiani na la MV Serengeti na kubainisha wazi kuwa MV Clarias ililalia upande mmoja ikiwa ghatini baada ya kutoka safari katika visiwa vya Gana na Goziba.

Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini ikiwa kulikuwa na uzembe au hujuma katika matukio yote mawili,endapo uchunguzi utaonesha uzembe au makosa ya watu, hatua kali zitachukuliwa ikiwemo watu kufikishwa mahakamani.

“MV Clarias ilikuwa na tatizo la matundu (Stain tube) yaliyo na upana usio wa kawaida, ya kuruhusu maji kuingia ndani ya meli na kupumua kwa kiwango kinachotakiwa.Uchunguzi unaendelea na hatua zitachukuliwa kwa wale watakaobainika kuhusika,” alisema Kaimu Mkurugenzi huyo wa TASHICO.

Naye, Said Sekiboto wa Kitengo cha Uokoaji Ndani ya Maji cha Jeshi la Zimamoto ya Uokoaji, Mkoa wa Mwanza, ameeleza kuwa hatua za dharura zinaendelea kuchukuliwa ili kuinyanyua meli ya MV Serengeti.

Amesema kuwa walifika katika tukio majira ya saa 8:00 usiku (Disemba 26,) baada ya kupata taarifa za meli hiyo kuzama, lakini walishindwa kufanya operesheni ya kuinyanyua mara moja kutokana na changamoto za vifaa.

“Vifaa tulivyokuwa navyo havikuwa na uwezo wa kuinyanyua meli kwa haraka, lakini sasa tumeimarisha vifaa hivyo na tunaendelea na operesheni ya kuinyanyua.Tutatumia vifaa vya ziada kuendelea na kazi ya kuinyanyua meli na kufyonza maji yaliyokuwa yamejaa ndani pamoja na kwenye Chelezo,”alisema.

Sekiboto ameongeza kuwa, licha ya meli hiyo upande wa nyuma kuzama hakuna madhara, sehemu ya mbele inaendelea kuelea juu ya maji, kazi ya kuondoa maji ndani ya meli itafanyika kwa siku nzima ili kuhakikisha usalama wa meli na kuirejesha hali yake.
Hivyo, TASHICO na vyombo vingine vya usalama, likiwemo Jeshi la Zimamoto, vinaendelea na operesheni hiyo kwa umakini mkubwa kuhakikisha meli inarejeshwa kwa usalama na kuondoa hatari yoyote inayoweza kutokea kwa umma na mali za serikali ili kusubiri uchunguzi zaidi wa kitaalamu.

AJALI YA GARI YAUA WATU SITA NYASA,WAMO WALIMU WANNE

 


Watu sita wamefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea katika Wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma
Ajali hiyo imetokea leo, tarehe 28 Desemba 2024, wakati wa safari kutoka kijiji cha Lumalu kilichopo katika Kata ya Upolo kuelekea makao makuu ya wilaya.
Akizungumza kwa njia ya simu, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Mheshimiwa Peres Magiri, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo, ambayo imesababisha vifo vya wafanyakazi wanne wa Serikali, wakiwa ni walimu wa Shule ya Msingi Lumalu.
Watu wawili wengine, wakiwemo dereva wa gari hilo na raia mmoja, pia amepoteza maisha.
Gari lililohusika katika ajali hiyo ni la aina ya Prado T 647 CVR, mali ya Vincent Alel Milinga kutoka kijiji cha Lumalu, Kata ya Upolo, Wilaya ya Nyasa.
Walimu waliopoteza maisha ni Damas Damasi Nambombe (Mwalimu),Domenica Abeat Ndau (Mwalimu),Judith Joseph Nyoni (Mwalimu),na John Silvester Mtuhi (Mwalimu).
Raia mwingine aliyefariki duni ni Boniface Bosco Mapunda pamoja na dereva wa gari hilo ambaye ni Vincent Alel Milinga.



 

MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR AWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA KILOMITA 28 KUADHIMISHA MIAKA 61 YA MAPINDUZI








Mazizini, Zanzibar – Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla, leo ameweka Jiwe la Msingi kwa Barabara ya Mazizini, Chukwani, na Maungani yenye urefu wa kilomita 28.164, ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kusherehekea miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Mradi huu wa barabara unalenga kuboresha miundombinu, kukuza uchumi wa wananchi, na kurahisisha huduma za usafirishaji katika maeneo haya. Akizungumza katika hafla hiyo, Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema kuwa hatua hii ni uthibitisho wa dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuboresha maisha ya wananchi kupitia maendeleo ya miundombinu.

"Barabara hii itakuwa kiungo muhimu kwa wakazi wa Mazizini, Chukwani, na Maungani, na itafungua fursa za kiuchumi na kijamii kwa maendeleo ya Zanzibar nzima," alisema Mheshimiwa Hemed.

Aidha, alitoa wito kwa wananchi kushirikiana na serikali katika kulinda miundombinu hiyo mara itakapokamilika ili iweze kudumu na kutimiza malengo yake.

Sherehe hizi ni sehemu ya kumbukumbu ya miaka 61 ya Mapinduzi Matukufu, yaliyotoa mwelekeo mpya kwa maendeleo ya Zanzibar.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
28 Desemba 2024

Thursday, December 26, 2024

Rais Samia Aendelea Kuwajali Watu Wenye Mahitaji Maalum kwa Sikukuu za Mwisho wa Mwaka






Zanzibar, Desemba 26, 2024 — Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mwanaidi Ali Khamis, amepongeza juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuonyesha upendo na kujali watu wenye mahitaji maalum nchini.

Akizungumza wakati wa kutoa zawadi za Sikukuu ya Christmas na Mwaka Mpya kwa niaba ya Rais Samia katika Makazi ya Wazee Zanzibar, Mhe. Mwanaidi amesema kuwa Rais Samia amekuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha watu wenye mahitaji maalum, hususan watoto na wazee, wanapatiwa huduma muhimu na mazingira bora ya kuishi.

"Mheshimiwa Rais ni kiongozi mwenye huruma na upendo kwa wananchi wote. Inapofika msimu wa sikukuu, ni kawaida yake kutoa zawadi kwa watoto, wazee, na wananchi wengine ili kuhakikisha wanafurahia kwa pamoja. Leo ameona ni vema kuwafikia wananchi wa Zanzibar," alisema Mhe. Mwanaidi.

Naibu Waziri aliwataka wananchi kote nchini kutumia msimu huu wa sikukuu kwa kuonyesha upendo na mshikamano kwa wenye mahitaji maalum kwa kuwasaidia mahitaji ya msingi na kuwapa faraja.

Alimalizia kwa kuhimiza jamii kushiriki kwa vitendo katika kuwajali wazee, watoto, na makundi maalum kwa ujumla, hasa wakati huu wa sherehe za mwisho wa mwaka.

Zoezi hilo limeleta tabasamu na faraja kwa wazee walioko katika makazi hayo, huku wakimshukuru Rais Samia kwa moyo wa huruma na mshikamano anaouonyesha mara kwa mara.


WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...