-Asema alikuwa alikuwa ni moja ya majaji wa mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa
WAZIRI
MKUU, Kassim Majaliwa leo Desemba 30, 2024 amemwakilisha Rais Dkt.
Samia Suluhu Hassan kwenye mazishi ya Mheshimiwa Mwanaisha Kwariko
ambaye alikuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani na Mjumbe wa Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi.
Akitoa Salama pole kwa waombolezaji nyumbani
kwa marehemu Kondoa, Mkoani Dodoma, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa
Rais Dkt. Samia ameguswa na kifo cha Mheshimiwa Mwanaisha kwani alikuwa
ni moja ya majaji wa mahakama ya rufani wenye uwezo mkubwa katika nafasi
zote alizozitumikia.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Marehemu
Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa kiongozi aliyetekeleza wajibu wake kwa
weledi na uadilifu “Msiba huu kwetu ni mzito, jukumu letu Wanakondoa,
Watanzania, Majaji na wajumbe wa Tume ni kuendelea kumuombea kwa
Mwenyezi Mungu”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa kila
mmoja kuenzi yote mazuri aliyoyafanya Mheshimiwa Mwanaisha katika
kipindi chake chote cha utumishi wa umma kwani kufanya hivyo kutakuwa ni
njia nzuri ya kuweka kumbukumbu ya kazi zake.
Kwa upande wake,
Jaji Mkuu wa Tanzania Profesa Ibrahimu Juma amesema kuwa Mheshimiwa
Mwanaisha Kwariko aliishi kiapo cha Uhakimu kwa kutoa huduma kwa
wananchi ikiwemo kutatua migogoro kwa uadilifu bila upendeo wowote,
“Mheshimiwa
Mwanaisha alikuwa na ubinadamu na utu, maisha yake yalikuwa ni
yakusaidia watu wengine, sisi tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwani uhai
wake umetusaidia sana katika shughuli mbalimbali za kimahakama”
Kwa
upande wake Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Mhe. Jaji
(Rufani) Jacobs Mwambegele amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha ameondoka
katika kipindi ambacho tume ilikuwa inamuhitaji hasa katika kipindi
hiki ambacho tume hiyo ipo katika mchakato wa kuboresha daftari la
kudumu la wapiga kura kuelekea uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na
Madiwani
“Tumempoteza Mheshimwa Mwanaisha tukiwa kwenye mzunguko
wa nane wa zoezi la kuboresha daftari na tukiwa tunaingia kwenye
mzunguko wa tisa utakaohusiaha mikoa minne Rukwa, Songwe, Njombe na
Ruvuma, pia mara zote alitoa ushauri wenye weledi wa hali ya juu katika
kuhakikisha tume inatekekeza majukumu yake kwa kuzingatia katiba sheria
kanuni na taratibu”.
Naye, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary
Senyamule amesema kuwa Mheshimiwa Mwanaisha alikuwa ni kiongozi mwenye
msimamo na mtetezi wa masuala ya wanawake, “alibobea katika eneo ambalo
alikuwa anafanyia kazi, sisi wanadodoma tutamkumbuka kwa machango wake
mkubwa kwenye masuala ya maendeleo”
Marehemu Mheshimiwa Jaji wa
Mahakama ya Rufani Mwanaisha Kwariko alifariki Desemba 27, 2024 nchini
India alipokuwa akipatiwa matibabu.