Thursday, September 15, 2016

WAZIRI WA AFYA AWAAGIZA MAKATIBU TAWALA KUTOA RUHUSA KWA MANESI KUFANYA UTAFITI WA AFYA

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (watatu kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar pamoja na wakufunzi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 mara baada ya kufunga mafunzo ya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 leo mkoani Dodoma. 
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu akihutubia leo mkoani Dodoma katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi wapatao 187 watakaofanya Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kuanza nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
 Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa akitoa maelezo ya kina kuhusu Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki ijayo.
 Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Dkt. Leonard Maboko akizungumza leo mkoani Dodoma wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 unaotarajia kufanyika nchi nzima kuanzia wiki ijayo. 
 Mratibu wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 Bi. Mariam Kitembe wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu akimkabidhi Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu kiasi cha Shilingi milioni moja na laki sita (1,600,000) zilizochangwa na wadadisi wa Utafiti huo kwa ajili ya waathirika wa Tetemeko lililotokea mkoani Kagera hivi karibuni. Mhe. Ummy Mwalimu amekabidhiwa fedha hizo wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo mkoani Dodoma. 
Baadhi ya wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 wakisikiliza kwa makini hotuba ya mgeni rasmi (hayupo pichani) wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya utafiti huo iliyofanyika leo mkoani Dodoma.
(Picha na Veronica Kazimoto).

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu amewaagiza Makatibu Tawala wa mikoa yote nchini kutoa ruhusa kwa manesi ambao ni wadadisi wa Utafiti wa Viashiria na Matokeo ya UKIMWI Tanzania wa mwaka 2016 ili kufanya utafiti huo.

Akizungumza leo katika hafla ya kuhitimisha mafunzo ya wadadisi hao iliyofanyika mkoani Dodoma, Waziri Ummy amesema utafiti huu ni wa muhimu sana hivyo Makatibu Tawala hawana budi kuwaruhusu manesi hao waliopata mafunzo kufanya utafiti huo.

“Ninawaagiza Makatibu Tawala wote nchini kuhakikisha wanatoa ruhusa kwa manesi mliopo hapa leo ili muweze kulisaidia taifa letu kwa kutuletea takwimu sahihi zitakazosaidia katika kutunga sera na kupanga mipango ya maendeleo hususani katika suala zima la afya”, ameagiza Mhe. Ummy Mwalimu.

Amefafanua kuwa, takwimu hizi zitasaidia kuboresha juhudi kubwa zinazofanywa na Serikali za kusogeza huduma zinazohusiana na VVU kama vile huduma za upimaji wa VVU bure katika vituo vya kutolea huduma za afya vya Serikali, kutoa huduma ya kupunguza maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto (PMTCT) pamoja na utoaji wa dawa za kupunguza makali ya VVU zijulikanazo kama ARV.

“Utafiti huu ni wa kipekee ukilinganisha na tafiti zingine zilizofanywa zinazohusu UKIMWI kutokana na kujumuisha upimaji wa homa ya ini ambao umekuwa tishio katika baadhi ya nchi barani Afrika”, amesisitiza Mhe. Ummy.

Aidha, Waziri Ummy ametoa wito kwa wananchi wote nchini kutoa ushirikiano kwa wadadisi watakaopita katika kaya mbalimbali zilizochanguliwa kwa ajili ya kufanya utafiti huu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Dkt. Albina Chuwa amesema utafiti huu utahusisha watu wote kwenye kaya zipatazo elfu kumi na sita (16,000) zilizochaguliwa kitaalam na kuwafikia watu wazima wapatao elfu arobaini (40,000) na watoto zaidi ya elfu nane (8,000).

Dkt. Chuwa ameeleza kuwa, takwimu hizi zitaisaidia Serikali katika kupanga na kusimamia utekelezaji wa sera mbalimbali zinazohusu sekta ya afya nchini hususani upatikanaji wa huduma za afya.
Wadadisi wapatao 187 ambao ni manesi kutoka hospitali mbalimbali nchini, wamemaliza mafunzo ya Utafiti wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI ambao unatarajia kuanza wiki ijayo.

Utafiti wa viashiria na Matokeo ya UKIMWI utahusisha upimaji wa UKIMWI, maambukizi mapya na wingi wa VVU mwilini kwa watu wanaoishi na VVU, wingi wa chembechembe za kinga mwilini (CD4 T-cell count), kiwango cha usugu wa dawa za ARV, kiwango cha maambukizi ya kaswende pamoja na homa ya ini (Hepatitis B na C).

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...