Tuesday, September 20, 2016

WAZIRI MKUU KASSIM MAJALIWA APOKEA MICHANGO YA SH. BILIONI MOJA

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea hundi ya shilingi 1,000,030,100/= kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi (katikati) na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru  (kushoto) kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi lililotokea Kagera .  Fedha hizo ni michango ya watumishi wa serikali na  Taasisi zake. Makabidhiano hayo yalifanyika Ofisini kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 20, 2016.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza baada ya kupokea hundi ya shilingi 1,000,030,100/= kutoka kwa  Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Mhandisi John Kijazi (katikati) na Msajili wa Hazina, Lawrence Mafuru   (wapili kulia) na Msajili wa Hazina Lawrence Mafuru  (kushoto) .Fedha hizo ni michango ya watumishi wa serikali na taasisis zake na makabidhiano yalifanyika Ofisni kwa Waziri Mkuu jijini Dar es salaam Septemba 20, 2016. 
(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea jumla ya sh. bilioni 1.040 kutoka kwa watumishi na wadau mbalimbali zikiwa ni misaada kwa wananchi walioathirika na tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera Septemba 10, mwaka huu.

Makabidhiano ya michango hiyo, yamefanyika leo mchana (Jumanne, Septemba 20, 2016) kwenye ukumbi wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es Salaam.

Akikabidhi hundi kwa Waziri Mkuu, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi alisema kiasi cha sh. 1,000,030,100 kimekusanywa kutoka kwa watumishi wa idara na Wizara zote  za Serikali na kwamba michango zaidi bado inaendelea kukusanywa.

“Tunaamini michango hii itasaidia kuwafuta machozi wenzetu waliopatwa na maafa japokuwa tunajua haitatosha kurudisha kile walichopoteza. Tuna imani itasaidia kupunguza makali ya machungu waliyoyapata,” amesema.

Hata hicyo, Balozi Kijazi amemhakikishia Waziri Mkuu kwamba bado wanaendelea kukusanya michango kutoka kwenye nyingine ambazo zilichelewa kupata taarifa na kwamba wakikamilisha wataiwasilisha mapema iwezekanavyo.
               
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amepokea michango ya sh. milioni 40 na kati ya hizo, sh. milioni 20 zimetolewa na kampuni ya ujenzi ya CHICO ya China na sh. milioni 20 nyingine zimetoka kwa Umoja wa Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa India waliopo nchini (India Business Forum).

Akiwasilisha mchango wake, Mwakilishi Mkuu wa kampuni ya CHICO hapa nchini, Bw. Guo Zhijian alisema wamesikitishwa na maafa yaliyotokea mkoani Kagera. “Tumefanya miradi mingi mkoani Kagera ikiwemo ujenzi wa barabara za urefu kilometa 300, kwa hiyo mkoa huu tunaujua zaidi. Tunatoa pole kwa wote waliopatwa na maafa  hayo,” amesema.

Naye Mwenyekiti wa umoja wa wafanyabiashara na wenye viwanda kutoka India (IBF), Bw. Gagan Gupta alimweleza Waziri Mkuu kwamba wameshtushwa na tukio hilo na kwamba wametanguliza kiasi hicho ili kisaidie juhudi za Serikali katika kukabiliana na maafa hayo.

“Bado tunaendelea kuwasiliana na wenzetu wengine na tukipata michango zaidi tutaiwasilisha mapema iwezekanavyo,” amesema.

Akitoa shukrani kwa waliotoa michango yote hiyo, Waziri Mkuu amewashukuru kwa misaada hiyo na kuahidi kuwa Serikali itahakikisha michango hiyo inafikishwa Kagera kwa walengwa.

“Tunashukuru sana kwa michango yote. Michango hii ni muhimu na inaonyesha mshikamano wa dhati uliopo. Michango hii inaonyesha kuguswa na mapenzi ya dhati kwa waliopatwa na maafa. Napenda niwahakikishie kuwa Kamati za Maafa za Mkoa, Ofisi ya Waziri Mkuu na kamati za wilaya, ziko pale kuhakikisha walengwa wanafikiwa,” ameongeza.

Waziri Mkuu amesema Serikali inakamilisha tathmini ya maafa hayo na kuahidi kutoa taarifa ya kiasi kilichokusanywa na kiasi kilichotumika. Amewaomba wananchi waliotoa ahadi zao za michango wakamilishe ahadi zao.

“Ninawaomba wale walioahidi kutoa michango wakamilishe ahadi zao na wale walio mbali na benki watumie namba za simu zilizotolewa mahsusi kwa ajili ya kuchangia maafa hayo,” amesisitiza.
Akaunti ya maafa imefunguliwa katika Benki ya CRDB yenye namba 015 222 561 7300 kwa jina la KAMATI MAAFA KAGERA – Swiftcode: CORUtztz na namba za simu za mkononi zinazotumika kupokea michango hiyo ni 0768-196-669 (M-Pesa) au 0682-950-009 (Airtel Money) au 0718-069-616 (Tigo Pesa).

Tetemeko hilo lililotokea Jumamosi, Septemba 10, mwaka huu, lilisababisha vifo vya watu 17 na wengine 440 kujeruhiwa. Kati yao, watu 253 walifikishwa Hospitali ya Mkoa, 153 walilazwa, 113 walitibiwa na kuruhusiwa na wengine 38 wanaendelea na matibabu ambapo kati yao watu 23 wamefanyiwa upasuaji mkubwa na wanaendelea vizuri.

Pia tetemeko hilo limesababisha nyumba 2,063 kuanguka huku nyingine 14,081 zikiwa katika hali hatarishi baada ya kupata nyufa na 9,471 zimepata uharibifu mdogo huku wananchi 126,315 wakihitaji misaada mbalimbali.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,
11410 - DAR ES SALAAM.

JUMANNE, SEPTEMBA 20, 2016.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...