Thursday, September 15, 2016

Waziri Mkuu Majaliwa: Aziagiza halmashauri zote nchini kutekeleza mpango kazi wa anwani za Makazi na Postikodi

 
Na Beatrice Lyimo na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Dodoma 
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kutekeleza mpango kazi wa anwani za Makazi na Postikodi kwa kushirikisha wadau mbalimbali wakiwemo wananchi. 

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa agizo hilo leo kabla ya kuzindua Mwongozo wa Mfumo wa Anwani za Makazi na Mwongozo wa Postikodi uliofanyika katika ukumbi wa Pius Msekwa uliopo ndani ya viwanja vya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dodoma. 

“Nikizingatia hatua ambazo zimechukuliwa na Serikali katika kuweka mazingira ya utekelezaji wa anwani za makazi, naagiza halmashauri zote nchini kuzifanyia kazi changamoto ambazo hazihitaji fedha ama ambazo hazihitaji gharama kubwa” amesema Waziri Mkuu Majaliwa. 

Waziri Mkuu amebainisha baadhi ya changamoto ambazo hazihitaji gharama kuwa ni pamoja na kuhakikisha barabara na mitaa yote inakuwa na majina yaliyorasimishwa na wananchi wenyewe, kudhibiti mipango miji dhaifu na ujenzi holela, kuwa na takwimu za idadi ya barabara na mitaa na nyumba katika kila kata na kuwa na taarifa za wakazi katika kila kata. 

Changamoto nyingine zisizohitaji gharama kubwa ni kujengea uelewa wadau na wananchi kuujua na kuwa mfumo huo, kuimarisha matumizi ya daftari la wakazi ambapo taarifa za utekelezaji wa kazi hizo Waziri Mkuu ameagiza ziwasilishwe Ofisi ya Rais TAMISEMI kabla ama ifikapo mwezi Desemba, 2016. 

Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa kufuatia nia ya Serikali kuhamia Dodoma, manispaa ya Dodoma na halmashauri ya Chamwino zipewe kipaumbele cha utekelezaji ili kuweka mazingira mazuri ya kuishi na kufanya kazi. 

“Utekelezaji wa Mpango katika Manispaa ya Dodoma na Halmashauri ya Chamwino ukamilike kabla ama ifikapo mwezi Desemba, 2016 na kuhakikisha utekelezaji huo kukamilika kwa wakati” amesema Waziri Mkuu Majaliwa. 

Kwa upande mwingine Waziri Mkuu amezitaka wizara za Ofisi ya Rais TAMISEMI, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Manispaa ya Dodoma, Halmashauri ya Chamwino, CDA; TCRA na TPC zishirikiane ipasavyo katika kukamilisha mpango wa anwani katika mkoa huo. 

Mbali na hayo, Waziri Mkuu amezitaka taasisi za TANROADS, TBA, NHC, Mipango Mji na Mradi wa Kuboresha Miji (TSC) zinapoandaa mipango hususan mipango ya miundombinu na makazi, ziainishe pia anwani za makazi kwa kushirikiana na Halmashauri katika maeneo husika. 

Katika kufanikisha hilo, Waziri Mkuu amezitaka Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Wizara ya Unjenzi, Uchukuzi na Mawasiliano na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, TCRA na TPC kushiriki ipasavyo katika utekelezaji wa mpango hususan katika kujenga uelewa na uwezo kwa viongozi na watendaji wa halmashauri ili waweze kutekeleza mpango huo ipasavyo. 

Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa George Simbachawene amesema kuwa Mpango huo umefanyiwa majaribio katika majiji mawili ya Dar es salaam na Arusha pamoja na manispaa za Dodoma na Zanzibar. 

Waziri Simbachawene aliongeza kuwa ili kuwa na Tanzania ya kisasa, anwani za makazi ni kigezo muhimu cha kuzingatiwa katika kundeleza majiji, manispaa, halmashauri, kata na hata mitaa ambayo ndio inajenga taswira ya nchi

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...