Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemtumia salamu za pongezi Rais Mteule wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein, kufuatia ushindi alioupata katika marudio ya Uchaguzi Mkuu wa Rais wa Zanzibar, uliofanyika jana tarehe 20 Machi, 2016.
Katika salamu hizo Rais Magufuli amesema ushindi wa Dkt. Shein umedhihirisha imani na matumaini makubwa waliyonayo wazanzibari kwake na kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Aidha, Rais Magufuli amewapongeza wananchi wa Zanzibar kwa kushiriki katika uchaguzi huo kwa amani na utulivu, na hatimaye kumpata mshindi wa kiti cha Urais ambaye atawaongoza kwa kipindi cha miaka mitano.
"Naomba nikupongeze kwa dhati Mheshimiwa Rais Mteule Dkt. Ali Mohamed Shein kwa ushindi ulioupata, ushindi ambao umeonesha kuwa wananchi wa Zanzibar bado wanahitaji uwaongoze kwa kipindi kingine cha miaka mitano" Amesema Rais Magufuli.
Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pia ameahidi kuwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kufanya kazi bega kwa bega na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) na amewataka Wazanzibari wote kujielekeza katika maendeleo kwa kuwa uchaguzi umekwisha.
"Ndugu zangu wa Zanzibar uchaguzi umekwisha, kilichobaki sasa ni kushirikiana na serikali yenu kuijenga Zanzibar na ninaamini mnao wakati mzuri wa kuijenga Zanzibar yenye maendeleo chini ya uongozi wa Dkt. Ali Mohamed Shein" amesisitiza Dkt. Magufuli
Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Dar es salaam
21 Machi, 2016
No comments:
Post a Comment