Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi (Kushoto) akizungumza wakati wa kuwasilisha taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma, katikati ni Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe na kulia ni katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof. Sifuni Mchome.Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe akipokea taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kutoka kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi.
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza mara baada ya kupokea taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kushoto ni Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi na kulia ni katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof Sifuni Mchome.
Picha zote na Raymond Mushumbusi MAELEZO
………………………………………………………………………………………
Na Jacquiline Mrisho -MAELEZO
Waziri wa Katiba na Sheria Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe amepokea taarifa ya utafiti wa marekebisho ya Sheria ya Manunuzi ya Umma kutoka Tume ya kurekebisha Sheria.
Akipokea taarifa hiyo leo Jijini Dar es salaam Mhe. Dkt.Harrison Mwakyembe amesema taarifa hiyo ya utafiti itasaidia kurekebisha sheria ya manunuzi ambayo inalenga kukuza uchumi wa nchi.
“Mimi na wataalamu wangu tumeipokea taarifa hii, tutaiangalia na kuhakikisha tunaifikisha Wizara ya Fedha na Mipango na kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuendelea na utaratibu unaofuata ili mchakato wa marekebisho uweze kufanyika kwa haraka”alisema Dkt Mwakyembe.
Akifafanua juu ya sheria ya manunuzi ya Umma, Mwenyekiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria Jaji Aloysius Mujulizi amesema kuwa Tume imefanya utafiti wa sheria hiyo kwa kushirikisha wadau mbalimbali.
“Tumepata maoni mengi na ushirikiano mkubwa kutoka kwa viongozi na wasimamizi wa manunuzi ya Serikali kwa namna wanavyoiona sheria ya manunuzi ya Umma,na sisi tumeyachambua maoni hayo kwa kutumia vigezo vya sheria”alisema Jaji Mujulizi.
Aidha,Tume imetoa maoni kwa Serikali kusimamia sheria ili iweze kuendana na ukuaji wa uchumi nchini kwa kurekebisha baadhi ya sheria ili kuepuka muingiliano uliopo kati ya sheria ya manunuzi na sheria nyingine.
Marekebisho ya sheria hii ni moja ya agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli lililotolewa Novemba 2015 alipokua akizindua Bunge la 11.
No comments:
Post a Comment