Tuesday, March 01, 2016

MKE WA RAIS MSTAAFU NA MWENYEKITI WA WAMA ASISITIZA UMUHIMU WA CHAMA CHA GIRL GUIDE TANZANIA KUONGEZA WANACHAMA

 Mke wa Rais Mstaafu na Mwenyekiti wa WAMA akisalimiana na Mama Othman Chande alipowasili katika Shule ya Sekondari Tambaza kuhudhuriaWorld Thinking Day iliyoandaliwa na Tanzania Girl Guide Association.
 Wanachama wa Girl Guide wakiwasili katika Shule ya Sekondari Tambaza  katika kusherekea World Thinking Day  ambao walipokelewa na Mgeni Rasmi Mama Salma Kikwete.
 Mama Salma Kikwete akiingia katika ukumbi wa Tambaza Sekondari akiwa na viongozi wa Girl Guide kushoto ni Mama Symphorosa Hangi, Kamishna Mkuu  na kulia ni Mama Matilda Balama na Mkuu wa Shule ya Tambaza.
Na Philomena Marijani- Meneja Uraghbishi na Mawasiliano, WAMA
CHAMA cha Girl Guide Tanzania kimetakiwa kuweka mikakati ya kuhakikisha inaongeza wanachama watakaojiunga na chama hicho ili vijana wengi waweze kunufaika.

Rai hiyo imetolewa mwishoni wa wiki na Mke wa Rais Mstaafu na  Mwenyekiti wa Taasisi ya WAMA, Mama Salma Kikwete wakati wa maadhimisho  ya kilele cha  siku ya  World Thinking Day yenye kauli mbiu ya Ungana, Shirikiana, Sherekea  iliyoadhimishwa na Tanzania Girl Guides Association. Sherehe hizo zilianza kwa maandamano ya wanafunzi Wanachama kutoka Upanga katika Makao Makuu ya Girl Guide Tanzania na kumalizikia  katika Shule ya Sekondari Tambaza ambapo  sherehe rasmi ilifanyika hapo.

Akiongea katika sherehe hizo Mama Salma Kikwete  alipongeza uongozi wa Girl Guide  kwa kufikia mikoa 19 ambapo  mpaka sasa chama kina  wanachama 97,143 na aliongeza kuwa changamoto kubwa waliyonayo ni kuongeza Wanachama zaidi kwani Tanzania ina watu wengi sana.

“Wito wangu kwenu ni kuongeza juhudi ya kuwafikia vijana wengi zaidi kwani sote tunajua umuhimu wa TGGA katika kuwasaidia vijana kujiepusha na changamoto mbalimbali katika makuzi yao. Ni lazima tuweke malengo ya muda mfupi, kati na mrefu ndani ya miaka mitatu ili ifikapo  mwaka 2018 tuwe tumeingiza wanachama zaidi ya 100,000/= Tumieni vizuri shule za msingi na sekondari , nina hakika mtafanikiwa kwa kiasi kikubwa sana. ” Alisema Mama Kikwete
Mama Kikwete pia alishauri uongozi wa Girl Guide Tanzania kubuni mbinu za kukabiliana na changamoto kwa kutumia rasilimali walizonazo.

“Kwa kuwa TGGA ni chama kikongwe, chenye rasilimali kama ardhi ambazo ziko sehemu nzuri kibiashara  naamini kwamba ikitayarishwa mipango mizuri  mnaweza kupata wabia wenye tija au mkawekeza kama chama kwa kushirikiana na mabenki. Mtakusanya kodi ambazo zitasaidia uendeshaji na kuongeza uwekezaji. ”Alisema Mama Kikwete.

Akielezea maana ya World Thinking Day Mkufunzi wa Taifa wa Tanzania Girl Guide Association, Mama Magreth Olumbe alisema kuwa sherehe hii ilianza rasmi mwaka 1926 ambayo ni siku ya; kuwakumbuka Girl Guide wote duniani na hasa wale walio kwenye mazingira magumu;kuongelea mambo yanayowagusa wasichana kwa mfano mimba za utotoni, kuolewa katika umri mdogo; na kukumbuka mwanzilishi wa Chama Lord Baden Powell na mke wake Olave Baden Powell.  

Akisoma risala kwa Mgeni Rasmi, Kamishna Mkuu wa  Tanzania Girl Guides Association, Mama Symphorosa Hangi alisema kuwa katika kuadhimisha  World  Thinking Day walikuwa na wiki mbili za kutoa huduma kwa jamii ikiwemo kuwatembelea wagonjwa katika hospitali ya Ocean Road na kutoa chakula, mavazi   na nauli za kuwarudishwa makwao wale waliokuwa wameruhusiwa baada ya matibabu. Aliongeza pia walitumia muda huo kuhamasisha wasichana wengine kujiunga na chama cha Tanzania Girl Guides ili nao waweze kupata fursa ya kujikwamua kifikra kwa kupitia mafunzo yanayotolewa na chama.
Chama cha Girl Guides Tanzania (TGGA) kilianzishwa hapa nchini mwaka 1928. TGGA ni chama kisicho cha serikali na ni cha kujitolea chenye lengo la kuwaendeleza watoto wa kike na wanawake kwa ujumla kushiriki katika maswala ya kijamii na kiuchumi kwa kupitia elimu na mafunzo yanayotolewa kwa kuzingatia kanuni za Girl Guides pamoja na kuwajenga kimaadili.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...