Sunday, May 25, 2008

Rais Kikwete safarini Japan

Rais Jakaya Mrisho Kikwete anaondoka nchini leo jioni (25 Mei, 08) kuelekea Japan kuhudhuria mkutano wa nne unaohusu maendeleo ya Afrika, ujulikanao kama Tokyo International Conference on African Development (TICAD) utakaofanyika katika jiji la Yokohama.

Kabla ya kuhudhuria mkutano huo, Rais Kikwete atafanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Japan Mhe. Yasuo Fukuda, tarehe 27 Mei, 08 kuzungumzia mahusiano na ushirikiano wa nchi mbili hizi katika maswala ya kiuchumi na kidiplomasia na pia kama Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Rais Kikwete anatarajiwa kumweleza mwenyeji wake juu ya maendeleo na changamoto mbalimbali zinazolikabili bara la Afrika na kujadili utatuzi wake.

Japan ni mshirika mkubwa wa maendeleo ya Tanzania ambapo Japan ni moja ya nchi zinazoisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ikiwemo kuchangia katika bajeti na pia imechangia katika misaada mbalimbali ikiwemo ya chakula, barabara na maji

Mkutano wa nne wa TICAD utaanza tarehe 28-30 Mei, ambapo viongozi wote wa bara la Afrika wamealikwa kuhudhuria pamoja na viongozi wa Japan, wakuu wa mashirika mbalimbali ya kimataifa duniani kama vile Umoja wa Mataifa, mashirika ya fedha duniani, taasisi sizizo za kiserikali kutoka bara la Asia na Afrika, nchi rafiki na wenza katika maendeleo duniani.

Mbali na mkutano wa TICAD Rais pia atashiriki mikutano na makongamano mbalimbali yanayohusu uchumi, miundo mbinu, maendeleo na maswala mbalimbali yanayohusu utunzaji wa mazingira barani Afrika na duniani kwa ujumla.

Aidha Rais Kikwete ataongoza mkutano utakaojadili tatizo la chakula duniani ambapo atazungumzia swala hili kwa kina hususan katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo hilo barani Afrika na hatimaye atashiriki katika kupitisha azimio la Yokohama.

Rais pia anatarajia kutumia nafasi hiyo kukutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Afrika watakaohudhuria mkutano huo.

Rais atafuatana na Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje, Mh. Benard Membe, Waziri wa Fedha - Mhe. Mustapha Mkulo, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Zanzibar - Mhe. Haroun Suleiman, Naibu Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko - Mhe. Cyril Chami na Mbunge wa Muleba Kusini na Mwenyekiti wa Kamati Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama - Mhe. Wilson Masilingi.

Rais anatarajiwa kurejea Dar-es-Salaam tarehe 31 Mei, 2008.


Imetolewa na Ikulu-Dar-es-salaam
25.05.08

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...