Thursday, May 29, 2008

Kikwete ateua wanawake saba majaji

KATIKA hatua ambayo inaonyesha azma ya kuziba pengo la majaji nchini, Rais Jakaya Kikwete, ameteua majaji 11 wapya ambao saba ni wanawake.

Uteuzi huo wa Rais licha ya kujaribu kuziba pengo la majaji, lakini pia umezidi kuongeza uwiano wa wanawake na wanaume katika nafasi za juu za maamuzi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, ikimnukuu Katibu Mkuu Kiongozi, Philemon Luhanjo, uteuzi huo umeanza Jumamosi iliyopita, Mei 24, 2008.

Rais amefanya uteuzi huo pia ikiwa ni takriban mwaka mmoja tangu ateue majaji wengine 20, ambao alifanya baada ya bunge la bajeti la mwaka jana.

Luhanjo katika taarifa hiyo ya Ikulu, aliwataja wanawake walioteuliwa kuwa majaji ni Sophia Wambura, Crecencia William Makuru, Zainabu Goronya Muruke na Upendo Hillary Msuya.

Wengine ni Atuganile Florida Ngwala, Rose Aggrey Teemba na Rehema Kiwanga Mkuye.

Majaji wengine wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni Kassim M. Nyangarika, Gabriel Kamugisa Rwakibarila, Ibrahim Sayida Mipawa na Lawrence Kisenge Nziajose Kaduri.

Katibu Mkuu Kiongozi ametangaza pia kwamba, Rais Kikwete amemteua Ferdinand Leons Katipwa Wambali, kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani.

Wambali anajaza nafasi iliyoachwa wazi na Wambura ambaye ameteuliwa kuwa Jaji wa Mahakama kuu ya Tanzania.

Kabla ya uteuzi wake, Wambali alikuwa Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama ya Rufani.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...