Kuelekea msimu mpya wa kilimo mwaka 2025/2026 kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imeendesha mafunzo ya matumizi sahihi ya mbolea kwa wakulima wa Mkoa wa Njombe, kata ya Makowo, ili kuongeza tija na uzalishaji.
Mafunzo hayo yaliyoanza kutolewa katika kijiji na Kata ya Makowo leo tarehe 2 Oktoba, 2025 yanalenga wakulima wa mazao mbalimbali yakiwemo ya kibiashara kama Viazi, Mahindi, Parachichi na Chai.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa TFRA, Joel Laurent, amesema elimu hiyo inalenga kuwajengea uwezo wakulima juu ya matumizi sahihi ya mbolea za kupandia, kukuzia na kubebeshea, ili kuepuka hasara na mavuno hafifu kutokana na kutokuzingatia matumizi sahihi ya mbolea. Matumizi sahihi ya mbolea yanaenda sambamba na utambuzi wa afya ya udongo na matumizi ya visaidizi vya mbolea.
Hata hivyo Mkurugenzi Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) ameahidi kupeleka kifaa cha upimaji afya ya udongo (Soil Scanner) Halmashauri ya Njombe mji ili kuwawezesha wataalamu kubaini mahitaji halisi ya udongo na kushauri aina bora ya mbolea kwa wakulima.
Kwa upande wake, Bwana Shamba wa kampuni ya mbolea ya OCP, Joshua Joel, amewataka wakulima kutumia mbolea kwa kuzingatia upatikanaji na zinazowawezesha kupunguza gharama za uzalishaji huku kampuni ikiwahakikishia wakulima kufikishia pembejeo hizo kwa wakati.
Wakulima walioshiriki mafunzo hayo, akiwemo Agnes Mgaya, Costa Abeck na Sabas Mwalongo, wameshukuru kwa kupewa elimu ya mbolea na kueleza imewapa mwanga mkubwa kwani awali walikuwa wakichanganya mbolea zaidi ya moja bila kufuata utaratibu wa kitaalamu jambo lililowapotezea rasilimali fedha.
Aidha, wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapa mbolea za ruzuku zilizopunguza gharama kubwa za uzalishaji na kueleza wanazipata kwa wakati katika maeneo yao.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji cha Makowo, Sabas Mwalongo, amewasisitiza wakazi wa eneo hilo kuhakikisha wanayafanyia kazi mafunzo waliyopewa ili yaweze kuwasaidia kufanya uzalishaji wenye tija kwa zao la viazi kwa kuwa ndiyo uchumi wa wananchi wa kata ya Mkowo.
Ameishukuru Serikali kwa kuwezesha mafunzo hayo kufanyika katika kijiji cha Makowo na Marimba, huku akiomba zoezi hilo liwe endelevu.
No comments:
Post a Comment