Sunday, October 26, 2025

RAIS DKT. MWINYI AKUTANA NA MISHENI YA UANGALIZI WA UCHAGUZI YA UMOJA WA AFRIKA
















Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo amefanya mazungumzo na Mkuu wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AUEOM), ambaye pia ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Botswana, Mheshimiwa Mokgweetsi Masisi, Ikulu Zanzibar. Mheshimiwa Masisi aliambatana na ujumbe wa maafisa waandamizi kutoka AUEOM walioko nchini kwa ajili ya kufuatilia maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania unaotarajiwa kufanyika hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi aliwakaribisha wageni hao na kuwapongeza kwa hatua ya Umoja wa Afrika kutuma timu ya waangalizi kama sehemu ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, amani na kwa kuzingatia misingi ya demokrasia barani Afrika.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha mazingira yote ya uchaguzi yanabaki kuwa salama na yenye amani, akisisitiza kuwa Zanzibar imejipanga vyema kwa zoezi hilo muhimu la kidemokrasia. “Hali ya ulinzi na usalama ni shwari, na wananchi wako tayari kushiriki kikamilifu katika uchaguzi,” alisema Rais Mwinyi.

Aidha, alibainisha kuwa Serikali inaendelea kushirikiana kwa karibu na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na wadau wengine ili kuhakikisha taratibu zote za uchaguzi zinafuatwa kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wao, ujumbe wa Misheni ya Uangalizi wa Uchaguzi ya Umoja wa Afrika (AUEOM) umepongeza hatua za maandalizi zilizochukuliwa na Serikali ya Zanzibar, hususan katika kuhakikisha mjumuisho wa makundi maalum ya jamii kama vile wanawake, vijana na watu wenye ulemavu katika mchakato wa uchaguzi.

Viongozi hao wamesema kuwa Umoja wa Afrika unaendelea kufuatilia mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi nchini Tanzania kwa lengo la kuhakikisha chaguzi zinazoendeshwa barani Afrika zinakuwa huru, haki na zenye uwazi. Wameongeza kuwa ni matarajio yao kuwa uchaguzi wa mwaka huu, Tanzania Bara na Zanzibar, utaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa nchi nyingine katika kudumisha amani, umoja na mshikamano wa kitaifa.

Mheshimiwa Masisi aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ukarimu na ushirikiano walioupata tangu walipowasili, akisisitiza kuwa ujumbe wake una imani kubwa na dhamira ya Tanzania ya kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa amani na kufanyika kwa misingi ya sheria na taratibu zote husika.

Mazungumzo hayo ni sehemu ya ratiba ya mikutano ya Misheni hiyo ya AUEOM na viongozi mbalimbali nchini, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya ufuatiliaji wa mchakato mzima wa uchaguzi wa mwaka 2025

No comments:

RAIS DKT. SAMIA AKUTANA NA UJUMBE WA JUKWAA LA MABUNGE LA NCHI ZA MAZIWA MAKUU (FP-ICGLR) IKULU NDOGO TUNGUU, ZANZIBAR

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Kiongozi wa Jukwaa la Mabunge la...