Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Dkt. Hassan Abbas leo Oktoba 17, 2025 ametembelea Hifadhi ya Taifa Mkomazi na kukagua mradi wa faru Mbula ikiwa ni moja ya ahadi alizozitoa Septemba 30, 2025 mara baada ya kukabidhi vitendea kazi katika kituo cha udhibiti wa wanyamapori waharibifu Goha wilayani Korogwe mkoani Tanga.
Katika ziara hiyo Dkt. Abbas alieleza kuwa zao la utalii ni matokeo chanya ya uhifadhi inayofanywa na maafisa na askari. Akiongea na TANAPA katika kikao kifupi Dkt. Abbas alisema,
"Ongezeko la Utalii ni matokeo ya Uhifadhi mnaufanya, tuzidi kushirikiana tusiishie tulipo, twende mbali zaidi kwa kutumia rasilimali zilizopo. Tuwekeze kwenye kujitangaza katika vivutio tulivyonavyo na siyo kujifungia ndani tukisubiri watalii waje ndipo wajifunze kujua mazao tuliyonayo. Tuwekeze kwenye maeneo ambayo tukiulizwa ndani ya miaka mitano au kumi ijayo ithibitishe uwekezaji tulioufanya umeleta tija na mapinduzi ya sekta ya utalii na uchumi kwa ujumla".
Aidha Dkt. Abbas aliongeza kuwa Wizara kupitia Jeshi la Uhifadhi linaendelea na mkakati wa kukusanya fedha kupitia Mfuko wa Uhifadhi wa Wanyamapori (TWDF) pamoja na Mfuko wa maendeleo ya utalii (TDl) itokanayo na mapato ya utalii mahifadhini na kutolewa kwa asilimia 3% hadi 6% kuilinda mifuko hiyo kwaajili ya kukuza utalii na uhifadhi. Pia amesema kuwa serikali imeongeza nguvu kwa kugawa vifaa na kuboresha miundombinu ili kutatua changamoto zinazokwamisha shughuli za uhifadhi.
Naye, Mkuu wa Kanda ya Kaskazini Naibu Kamishna wa Uhifadhi Steria Ndaga, alimkaribisha Katibu Mkuu na kumshukuru kwa jitihada zote zinazofanyika kuunga mkono maendeleo ya sekta ya uhifadhi na utalii yenye mchango mkubwa katika ongezeko la pato la Taifa nchini.
Akiwasilisha taarifa fupi ya Hifadhi Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Emmanuel Moirana alitoa takwimu na kuonesha kuwa Hifadhi ya Taifa Mkomazi inapiga hatua katika ongezeko kubwa la watalii toka idadi ya watalii 489 kwa mwaka 2015/2016 na hadi kufikia idadi ya 10991 kwa mwaka 2024/2025.
Mara baada ya kikao hicho Dkt. Abbas alipata nafasi ya kutembelea mradi wa Faru Mbula wenye Kilometa za mraba 13 na kujionea faru 9 kati ya 13 waliomo katika mradi huo.
No comments:
Post a Comment