Wednesday, October 01, 2025

NHC Yazindua Mauzo ya Nyumba Dar, Tanga na Tabora





Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limezindua rasmi mauzo ya nyumba katika miradi mikubwa ya kisasa jijini Dar es Salaam na mikoa ya Tanga na Tabora. 

Uzinduzi huo umefanyika Makao Makuu ya NHC, Kambarage House, ukiongozwa na Meneja Mauzo na Masoko, Deogratius Batakanwa, ambaye amesema hatua hii inalenga kuhakikisha Watanzania wanapata makazi bora, ya kisasa na yenye thamani ya kudumu.
 
Amesema kuwa Jijini Dar es Salaam, NHC imezindua mauzo ya nyumba kwenye mradi wa Boulevard Residence yenye nyumba za chumba kimoja (37.7 sqm), vyumba viwili (103.5 sqm) na vyumba vitatu (124.2 sqm), Katika mradi huu mauzo yanaanzia shilingi milioni 248 yakiwa na VAT.
 
Kwa upande wa nyumba za mradi wa Samia Housing Kijichi Residence wenye nyumba za chumba kimoja (32.02 sqm), vyumba viwili (62.70 sqm) na vyumba vitatu (95.30 sqm). Katika mradi huu mauzo yanaanzia shilingi milioni 112 yakiwa na VAT. 
 
Kwa mkoa wa Tanga, NHC inatangaza mauzo ya nyumba mradi wa  Mkwakwani Plaza zenye vyumba viwili (80 sqm) na vitatu (108 sqm),Katika mradi huu mauzo yanaanzia shilingi milioni 185 yakiwa na VAT, huku mkoani Tabora ikitangaza kuuza nyumba kwenye mradi wa Tabora Plaza yenye vyumba viwili (95 sqm) na vitatu (124 sqm). Katika mradi huu mauzo yanaanzia shilingi milioni 225 yakiwa na VAT.
 
Bei za nyumba hizi zimepangwa kwa kuzingatia mahitaji ya Watanzania wa kipato tofauti, na lengo kuu ni kutoa fursa kwa kila mmoja kumiliki nyumba bora. Wateja wanaweza kupata huduma kwa kupiga namba ya huduma 0736 114 433 au kuwasiliana moja kwa moja na maafisa mauzo walioteuliwa.
 
Batakanwa amesema NHC itaendelea kujenga taifa kwa kutoa makazi bora na kuwataka Watanzania kutumia fursa ya kipekee ya kumiliki nyumba katika maeneo yenye miundombinu bora na mazingira salama. 
 
Kupitia miradi hii, NHC imeonesha dhamira ya kuharakisha maendeleo ya makazi nchini na kuwapa wananchi fursa ya kuishi na kufanya biashara katika mazingira ya kisasa.
 

No comments:

UJIRANI MWEMA KATI YA NGORONGORO NA VIJIJI VYA JIRANI WAZIDI KUIMARISHWA

  Na Mwandishi Wetu Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, Joas...