Wednesday, October 08, 2025

TANAPA YAZINDUA RASMI APP YAKE KUPANUA UTALII DUNIANI












Na. Calvin Katera - Mikumi

Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limezindua rasmi Programu Tumizi "App" yake Leo Oktoba 08, 2025 katika viwanja vya Hifadhi ya Taifa Mikumi ikilenga kupanua wigo wa utalii kwa kurahisisha upatikanaji wa taarifa za vivutio vya hifadhi zote za Taifa nchini. 

Akizindua Programu hiyo Tumizi Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Hassan Abbas ambaye ni Mgeni rasmi amepongeza juhudi hizo za kutangaza utalii kupitia teknolojia  hasa ile inayopatikana katika simu janja ya kiganjani huku akitoa Takwimu za watumiaji wa simu janja za viganjani pamoja na intaneti duniani.

"Dunia ina jumla ya watu Bilioni nane Watu zaidi ya Bilioni tano wanatumia simu za mkononi na kati ya watumiaji hao asilimia 87% wana simu janja. Na watu Bilioni 5.7 ni watumiaji wa intaneti duniani. Hivyo basi "App" hii inakuja wakati muhimu sana leo kwani inaenda kutatua changamoto yetu kubwa ya kujitangaza katika soko la utalii duniani. Programu tumizi hii itaturahisishia mambo mengi, inatusaidia kujua fursa za uwekezaji zinazopatikana katika hifadhi zote za Taifa nchini, kadhalika taarifa rasmi za hifadhi husika bila ukakasi". 

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Mkuu wa Majeshi Mstaafu Jenerali George Waitara amesema kuwa Programu hiyo tumizi "App" itaongeza ufanisi katika shughuli za Utalii na Uhifadhi na kuipongeza Menejimenti ya Shirika kwa kuendana na mabadiliko ya teknolojia ya TEHAMA

"Nimekuwa nikiwaambia hakuna kinachoshindikana ni kudiriki na uthubutu. Niwapongeze Menejimenti ya TANAPA kwa ubunifu huu wa Programu Tumizi "App" hii ya "TANAPA GO" itaimarisha utendaji wa Shirika na kuwa wa haraka na wenye ufanisi mkubwa kwani huduma pamoja na taarifa mbalimbali zitawafika wageni wa  ndani na nje ya nchi. Kazi kubwa mmeifanya kwa pokeeni pongezi za Bodi ya Wadhamini".

Awali, akitoa neno la Utangulizi Naibu Kamishna wa Uhifadhi Maendeleo ya Biashara TANAPA Masana Mwishawa ameeleza kuwa Programu Tumizi hiyo ni daraja kubwa katika kuongeza na  kukuza maendeleo ya sekta ya uhifadhi na Utalii. App hii (TANAPA GO)  itachangia kwa upana upatikanaji wa taarifa za Hifadhi kwa wepesi kwa watalii wote wanaotembelea au wanaopanga kutembelea Hifadhi za Taifa nchini.

No comments:

TANAPA YAZINDUA RASMI APP YAKE KUPANUA UTALII DUNIANI

Na. Calvin Katera - Mikumi Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), limezindua rasmi Programu Tumizi "App" yake Leo Oktoba 0...