Friday, October 17, 2025

DKT. KIKWETE NA MAKAMU WA RAIS DKT. MPANGO WASHIRIKI KUAGA MWILI WA RAILA ODINGA NAIROBI









Rais mstaafu wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, pamoja na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, wameshiriki kushiriki kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu wa Kenya, Mhe. Raila Amolo Odinga, aliyefariki akiwa Nchini India tarehe 15 Oktoba 2025. Mazishi hayo ya kitaifa yamefanyika leo tarehe 17 Oktoba 2025, katika Uwanja wa Nyayo, Jijini Nairobi.

Katika hafla hiyo, Dkt. Mpango alimfariji Rais wa Kenya, Mhe. Dkt. William Ruto, kufuatia msiba mkubwa uliogusa mioyo ya Wakenya na wananchi wa Afrika Mashariki. Kwa upande wake, Dkt. Kikwete ni miongoni mwa waombolezaji waliokusanyika kushiriki kumuaga Odinga, akionesha heshima ya dhati kwa marehemu ambaye hakuwa tu mwanasiasa, bali pia mshirika wa dhati katika juhudi za kudumisha amani, demokrasia na mshikamano barani Afrika.

Kumbukumbu za kihistoria zinaonesha jinsi Rais Kikwete alivyojenga uhusiano wa karibu na Kenya, hususan mwaka 2008 alipokuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, wakati Kenya ilikumbwa na mgogoro wa kisiasa uliosababisha vifo na machafuko makubwa. Wakati huo, Dkt. Kikwete, akiwa sambamba na Hayati Kofi Annan na Hayati Benjamin Mkapa, alishiriki moja kwa moja katika mchakato wa usuluhishi wa kisiasa uliomleta pamoja Rais Mwai Kibaki na Raila Odinga, hatua iliyorejesha amani na kuzaliwa kwa Serikali ya Maridhiano.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, Dkt. Mpango alieleza kuwa marehemu Raila Odinga alikuwa kiongozi shupavu, mzalendo na mtetezi wa haki za watu, ambaye mchango wake utaendelea kukumbukwa katika historia ya ukombozi wa kisiasa na maendeleo ya bara la Afrika.

Mazishi hayo yameakisi umoja, heshima na ujirani mwema uliopo kati ya Tanzania na Kenya, huku ujumbe wa amani, mshikamano na upendo ukitawala hafla hiyo ya kihistoria.

#RailaOdinga #DktKikwete #DktPhilipMpango #WilliamRuto #KenyaTanzaniaUnity #UjiraniMwema #AfricaPeace #UmojaWaAfrika

No comments:

CHUO KIKUU MZUMBE CHAPOKEWA MSAADA WA VITABU KUTOKA ACCA

  Chuo Kikuu Mzumbe kimepokea vitabu 69 vya kufundishia na kujifunzia kutoka Association of Chartered Certified Accountants (ACCA) kupitia o...