Na Mwandishi Wetu
Naibu Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayesimamia Uhifadhi, Utalii na Maendeleo ya Jamii, Joas Makwati, ameongoza kikao cha ujirani mwema na viongozi wa vijiji vinavyopakana na hifadhi hiyo mnamo Oktoba 1, 2025, ambapo alisisitiza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano kati ya wananchi na Mamlaka hiyo.
Katika kikao hicho kilichohusisha viongozi wa vijiji vya Wilaya za Karatu na Monduli, Makwati aliambatana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Bi. Gloria Bideberi, pamoja na watendaji wengine waandamizi wa Mamlaka.
Viongozi wa vijiji waliwasilisha changamoto mbalimbali zinazowakabili wananchi, kubwa ikiwa ni uvamizi wa wanyamapori wakali na waharibifu – hususan tembo na nyati – wanaoingia makazi na mashamba na kusababisha uharibifu wa mazao. Walisema hali hiyo imekuwa tishio kwa usalama na maendeleo ya kiuchumi ya kaya nyingi zinazotegemea kilimo kama njia kuu ya kujipatia kipato.
Akizungumza baada ya majadiliano hayo, Naibu Kamishna Makwati alisema kikao hicho ni hatua muhimu ya kuimarisha ujirani mwema na kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti changamoto zinazojitokeza baina ya binadamu na wanyamapori.
“Tunapaswa kushirikiana kwa karibu ili kulinda hifadhi na wakati huo huo kulinda maisha na mali za wananchi. Huu ni mwanzo mzuri wa kujenga uelewano endelevu,” alisema Makwati.
Kwa upande wake, Bi. Bideberi alisisitiza kuwa Mamlaka itaendelea kushirikiana na wananchi kupitia vikao vya majadiliano na mipango ya pamoja ya kijamii ili kuhakikisha jamii za jirani na hifadhi zinanufaika zaidi na uwepo wa hifadhi hiyo.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro imekuwa ikiendesha ziara na mikutano katika vijiji mbalimbali ili kusikiliza changamoto za wananchi na kuimarisha mahusiano ya ujirani mwema, lengo likiwa ni kulinda maliasili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.