Ujenzi wa Soko la Madini la Tanzanite Trading Centre lililopo Mirerani, wilayani Simanjiro mkoani Manyara, umefikia asilimia 98 na unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti mwaka huu.
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga, alitoa agizo hilo jana Agosti 18, 2025 wakati akiweka jiwe la msingi la mradi huo, akimtaka mkandarasi wa ujenzi huo, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), kuhakikisha jengo linakamilika mapema kabla ya kuanza kwa shughuli rasmi za kibiashara.
“Hakuna sababu ya kuchelewesha mradi huu, hasa ikizingatiwa kuwa Rais wetu, Mhe. Samia Suluhu Hassan, tayari ametoa zaidi ya shilingi bilioni 5.5 kwa ajili ya kukamilisha soko hili,” alisema RC Sendiga.
Aidha, alielekeza kuwa kufikia Septemba 15, 2025, shughuli za uuzaji na uchakataji wa madini zianze rasmi katika soko hilo, akibainisha kuwa litakuwa chachu ya mabadiliko ya kiuchumi na kijamii kwa wananchi wa Mirerani na wilaya ya Simanjiro kwa ujumla.
Katika hatua za maandalizi, RC Sendiga alimwagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Simanjiro kuhakikisha maboresho ya ndani na nje ya eneo la soko yanakamilika kwa wakati, huku akisisitiza kuwa viwanja vya biashara vinavyozunguka eneo hilo vitolewe kwa wananchi bila urasimu.
“Viwanja hivi ni mali yetu wananchi wa Mirerani. Tuelezwe wazi masharti ni yapi ili wananchi wajipange mapema. Tunataka faida ya kwanza ibaki kwa wananchi wa hapa,” alisisitiza.
Vilevile, aliwataka viongozi na wananchi kushirikiana katika kulitangaza soko hilo ili liwe kitovu cha biashara na uwekezaji wa madini aina ya Tanzanite, ambalo ni kivutio cha pekee duniani.
Katika wito mwingine, RC Sendiga aliwakumbusha wakazi wa Mirerani na Simanjiro kwa ujumla kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani utakaofanyika Oktoba 29, 2025.
No comments:
Post a Comment