Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuonesha dhamira ya kukuza uchumi wa nchi kwa vitendo baada ya kufungua rasmi Kituo cha Biashara na Usafirishaji Afrika Mashariki (EACLC) kilichopo Ubungo, jijini Dar es Salaam leo tarehe 1 Agosti 2025.
Kituo hicho ni cha aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki, kikilenga kuwa kitovu cha biashara, usafirishaji na huduma za kisasa, chenye uwezo wa kuhudumia wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi kwa ufanisi mkubwa.
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Mhe. Rais Samia alisisitiza kuwa mradi huu ni sehemu ya ajenda ya Serikali ya Awamu ya Sita ya kuwezesha biashara, kuhamasisha uwekezaji na kupanua fursa za ajira kwa Watanzania.
“Kituo hiki si tu miundombinu ya kisasa, bali ni jukwaa la mawasiliano ya kibiashara kati ya Tanzania na nchi jirani. Ni chachu ya ukuaji wa biashara ndogo, za kati na kubwa, huku tukijenga mazingira rafiki kwa wawekezaji,” alisema Rais Samia.
Umuhimu wa Kituo cha EACLC:
Kituo hiki kinatarajiwa kuongeza mnyororo wa thamani wa biashara za kikanda, kwa kurahisisha upatikanaji wa huduma mbalimbali kwa wafanyabiashara na wasafirishaji. Pia, kitasaidia kuharakisha na kuimarisha usalama wa usafirishaji wa bidhaa, hali itakayoboresha ushindani wa Tanzania katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Vilevile, kwa kutoa huduma bora, kituo hiki kitawavutia wawekezaji wa kimataifa, jambo litakalosaidia kukuza uchumi wa taifa. Kwa ujumla, mradi huu mkubwa utatoa maelfu ya ajira kwa Watanzania, moja kwa moja na kwa njia zisizo za moja kwa moja, hivyo kuchochea ustawi wa jamii na maendeleo ya nchi.
No comments:
Post a Comment