📍Dodoma, Tanzania
Serikali imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha Watanzania kupitia uongezaji thamani ndani ya nchi ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha uchumi wa kijani (green economy) hususan katika utengenezaji wa magari ya umeme, betri za magari, nishati safi na vifaa vya kielektroniki.
Hayo yamewekwa wazi leo Agosti 26, 2025 na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, wakati akiweka jiwe la msingi la Kiwanda cha kusafisha na kusindika Madini ya Nikeli na Shaba kinachojengwa na Kampuni ya Zhongzhou Mining Co. Ltd, eneo la Zamahero, Wilaya ya Bahi, mkoani Dodoma.
Amesema kuwa, Mradi huo utekelezaji wa maelekezo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwamba madini yanayochimbwa hapa nchini yaongezewe thamani ndani ya nchi na kuuza bidhaa ya mwishyabadala ya madini ghafi.
“Ujenzi wa kiwanda hiki ni uthibitisho kuwa dhamira ya kuongeza thamani madini nchini, tunataka kuona Tanzania ikibadilika na kuwa taifa linalozalisha bidhaa zenye thamani kubwa kwenye soko la dunia la bidhaa teknolojia.” amesema Mavunde
Waziri Mavunde ameeleza kuwa mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani milioni 15 utakapokamilika utazalisha takribani tani 200,000 za nikeli na shaba kwa mwaka, kuajiri zaidi ya Watanzania 200 hadi 230, na kuchangia kodi na mapato mengine ya Serikali.
“Uwekezaji huu ni kielelezo cha mafanikio ya Serikali katika kufanikisha dira ya uchumi wa viwanda na uongezaji thamani madini kama ilivyoelekezwa na Ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020–2025," amesisitiza Mavunde.
Amebainisha kuwa, pia Sera ya Madini ya mwaka 2009 inaelekeza kuyaongezea thamani madini yetu ndani ya nchi na kuongeza kuwa “hivi sasa Tanzania tuna viwanda vinane vya kusafisha madini ya dhahabu (gold refinery) lakini viwanda vya kuongezea thamani Madini ya metali tunavyo 9, mkoa wa Dodoma peke yake tunavyo vitano” ameongeza Mavunde.
Kwa upande wake, Kamishna wa Madini, Dkt. AbdulRahman Mwanga amesema kuwa, kwa kuwekeza kwenye miradi ya kuongeza thamani, Tanzania inajenga msingi imara wa ajira, mapato, na uchumi shindani kimataifa na kufikia lengo la ujenzi wa Tanzania ya uchumi.
Naye, Mkurugenzi wa Kampuni ya Zhongzhou Mining Lee Zhong LIANG amemuhakikishia Waziri Mavunde kuwa Kampuni itaendeleza uhusiano mwema na Serikali pamoja wananchi wanaozunguka mradi huo.
Pia, Katibu Tawala Wilaya ya Bahi , Mwanamvua Muyongo ameeleza kuwa uwepo wa kiwanda hicho utasaidia kuiweka Wilaya hiyo katika ramani ya wazalishaji wa bidhaa muhimu za kiteknolojia pamoja na kuboresha maisha ya watu wa hapa kupitia ajira rasmi na zisizo za moja kwa moja.
*#Value Addition
For Socio- Economic Development*
#Uongezaji Thamani Madini kwa Maendeleo ya Kiuchumi na Kijamii
No comments:
Post a Comment