Dar es Salaam, 14 Agosti 2025
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ametunukiwa Nishani ya Heshima ya Juu ya Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani, inayojulikana kama The Grand Cordon. Hafla ya kutunuku heshima hiyo imefanyika leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, ikiakisi mchango wa kipekee wa Rais Samia katika kuunga mkono na kuendeleza michezo ya majeshi kitaifa na kimataifa.
Nishani hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa Baraza la Michezo ya Majeshi Duniani (CISM) kwa Kanda ya Afrika, Meja Jenerali Maikano Abdullahi kutoka Nigeria, kwa niaba ya Baraza hilo. Tukio hilo limehudhuriwa na viongozi waandamizi wa Serikali, maafisa wakuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), pamoja na wawakilishi wa CISM.
Katika hotuba yake ya shukrani, Mhe. Rais Samia ameishukuru CISM kwa kutambua mchango wa Tanzania katika michezo ya kijeshi, akisisitiza kuwa michezo ni nyenzo muhimu ya kuimarisha umoja, mshikamano, na mawasiliano mazuri kati ya majeshi ya mataifa mbalimbali. Aidha, ameeleza dhamira ya Tanzania kuendelea kushiriki kikamilifu katika mashindano ya kijeshi ya kimataifa na kuendeleza vipaji vya wanamichezo kutoka vikosi vyake.
Kwa upande wake, Meja Jenerali Maikano Abdullahi amempongeza Rais Samia kwa uongozi wa mfano na kwa kutoa kipaumbele cha kipekee katika kuinua michezo kama sehemu ya ustawi wa majeshi na diplomasia ya kijeshi. Alisisitiza kuwa tuzo ya The Grand Cordon hutolewa kwa viongozi wachache duniani waliotoa mchango wa kipekee katika kukuza mshikamano wa wanajeshi kupitia michezo.
Nishani ya The Grand Cordon ni heshima ya juu kabisa inayotolewa na CISM, ikiwakilisha utambuzi wa heshima kubwa kwa mchango wa kiongozi katika michezo ya kijeshi. Tanzania ni miongoni mwa nchi chache barani Afrika ambazo viongozi wake wamepata heshima hii.
No comments:
Post a Comment