Monday, August 11, 2025

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango Ahimiza Ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Wadau wa Uchaguzi kwa Amani na Usalama











Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano wa karibu na wadau wote wa uchaguzi ili kuhakikisha haki zinatendeka kwa kila mdau na kuondoa tofauti zozote zinazoweza kusababisha migongano.

Kauli hii imetolewa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Maafisa Waandamizi wa Jeshi la Polisi unaofanyika katika ukumbi wa Chuo cha Polisi (CCP) Moshi, Mkoani Kilimanjaro. Dkt. Mpango amesema maeneo muhimu ya ushirikiano ni pamoja na kuhakikisha mikutano ya kampeni inafanyika katika maeneo na muda ulioruhusiwa, kuzuia maandamano yasiyo na kibali, kuimarisha usalama wa wagombea na viongozi wa vyama vya siasa bila ubaguzi wowote, pamoja na kudhibiti misongamano mikubwa ili shughuli nyingine za kijamii na kiuchumi ziendelee bila usumbufu.

Aidha, Makamu wa Rais alitoa wito kwa Jeshi la Polisi kushirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na taasisi nyingine za Serikali ili kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) kufuatilia na kuchambua taarifa zenye mlengo wa uchochezi zinazotolewa kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. 

Aliongeza kuwa matumizi ya teknolojia za akili bandia yanawawezesha baadhi ya watu kusambaza picha na video za uongo za wagombea, jambo linaloweza kuhatarisha amani na utulivu wa jamii.

Jeshi la Polisi limehimizwa kujiandaa kikamilifu kufanya doria ya mtandao ili kubaini na kuchukua hatua za haraka kisheria dhidi ya machapisho yanayokiuka sheria. Vilevile, ushirikiano na TAKUKURU na vyombo vingine vya usalama unahitajika ili kudhibiti vitendo vya rushwa kipindi cha uchaguzi. Polisi Jamii pia inatakiwa kushirikiana na TAMISEMI kuhakikisha usalama ngazi za kata, shehia, vijiji na mitaa.

Dkt. Mpango amesisitiza Jeshi la Polisi lisimamishe utekelezaji wa sheria za uchaguzi na sheria nyingine za nchi kwa weledi na uadilifu, na kuwahimiza wananchi pamoja na viongozi wa vyama vya siasa kuepuka kujichukulia sheria mkononi bali kutoa taarifa kwa vyombo vinavyostahili.

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuwajengea uwezo maafisa na askari kwa mafunzo ya utayari, uadilifu na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao. Alimpongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Camillus Wambura, kwa kuhakikisha askari wanapata mafunzo ya kitaalamu.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, ameishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwapa wizara hiyo bajeti na vifaa vya kisasa vinavyosaidia kuboresha utendaji kazi wa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya usalama. 

Ameahidi kuwa wizara na vyombo vyote vya usalama vitaendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, nidhamu, weledi na uadilifu kuhakikisha nchi inakuwa na amani, usalama na mazingira mazuri kwa maendeleo endelevu.

Awali, IGP Camillus Wambura alihakikisha kuwa Jeshi la Polisi limejipanga vyema kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu. Alisema kauli mbiu ya mkutano huo ni “Amani, Utulivu na Usalama kabla, wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu 2025 ni jukumu letu sote.” Amesisitiza kuwa jukumu la kulinda amani na usalama ni la kila Mtanzania kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Mkutano huo wa siku tano unafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 15 Agosti 2025, ukiangazia usalama, utulivu na ufanisi katika mchakato wa uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

No comments:

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango Ahimiza Ushirikiano wa Jeshi la Polisi na Wadau wa Uchaguzi kwa Amani na Usalama

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango, amesisitiza umuhimu wa Jeshi la Polisi kuimarisha ushirikiano wa...