Monday, March 03, 2025

WAKULIMA WANEEMEKEA NA ZAO LA KAHAWA,WASEMA MIKOPO YA PEMBEJEO IMEWASAIDIA KULIMA KWA TIJA


Na Mwandishi Wetu,Ruvuma

WAKULIMA wa zao la kahawa wanaohudumiwa na Chama cha Msingi cha Ushirika KImuli Amcos kata ya Utiri Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma, wamefanikiwa kuzalisha tani 105,986.95 za kahawa zilizowaingizia zaidi ya Sh.bilioni 14,022,174,698.40 kuanzia Msimu wa kilimo 2021/2022 hadi 2024/2025.

Katibu wa Chama hicho Aron Komba amesema,katika msimu 2021/2022 wakulima walizalisha tani 548,551 zenye thamani ya Sh.bilioni 3,299,453,120,msimu wa kilimo 2022-2023 walizalisha tani 455,643 ambazo ziliwaingizia Sh.bilioni 3,065,405,776.40.

Aidha alisema,msimu wa 2023/2024 Wakulima ambao ni Wanachama wa Kimuli Amcos walizalisha jumla ya kilo 585,288 zenye thamani ya Sh.bilioni 2,929,893,908 na msimu 2024/2025 walizalisha kilo 530,253 ambazo waliuza Sh.bilioni 4,727,421,894 kupitia njia ya minada.


“Pia kwa muda wa miaka minne ya Uongozi wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,tumetoa mikopo ya pembejeo yenye thamani ya Sh.bilioni 3,056,783,867 kwa Wakulima 7,005 wanaojishughulisha na kilimo cha kahawa na mazao mengine ya chakula na biashara”alisema Komba.

Kwa mujibu wa Komba,msimu wa kilimo 2022/2023 wametoa mikopo ya pembejeo ya Sh.957,343,812 kwa wanachama 2,137 mwaka 2023/2024 Sh.917,834,200 kwa Wanachama 2,381 na mwaka 2024/2025 wametoa mikopo yenye thamani ya Sh.1,181,605,855 iliyokwenda kwa Wananchama 2,487.


Alisema,mikopo hiyo imewasaidia Wanachama kulima kwa tija na kuongeza uzalishaji kwani hapo awali walikuwa wanaangaika kutafuta pembejeo ambazo ziliuzwa kwa bei kubwa kati ya Sh.165,000 hadi 170,000 kwa mfuko mmoja wa kilo 25.

Alisema,hali hiyo ilipelekea baadhi ya wakulima kukata tamaa na kutoendelea na shughuli zao za kilimo kutokana na kushindwa kumudu gharama ya pembejeo ambapo, amempongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan,kwa kuanza utaratibu wa kutoa pembejeo za ruzuku kwa zao la kahawa.

Komba,ameiomba Serikali kuendelea kutoa pembejeo za ruzuku kwa zao la kahawa ili kuwapunguzia wakulima mzigo mkubwa wa kununua pembejeo kwa bei ya juu na kuongeza upatikanaji wa pembejeo za ruzuku ili wakulima waweze kuzalisha kwa wingi.

“Naishauri Serikali kama inataka kufanikisha mpango wake wa kutouza kahawa ghafi basi ituwezeshe kwa kutujengea miundombinu ili tuweze kukaanga kahawa tunayozalisha kwa ajili ya matumizi ya sisi wenyewe na watu wengine na nyingine tuuze kwenye soko la nje"alise
ma Komba.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Amcos ya Kimuli Yordan Komba alisema,katika kipindi cha miaka minne Chama hicho kimepiga hatua kubwa kwa kuongeza Wanachama kutoka 364 tangu kilipoanzishwa mwaka 1993 hadi 1,700 mwaka 2024.

Aidha,ameiomba Serikali kupitia maafisa Ugani kwenda kwa wakulima kuwapa utaalam na mbinu za kilimo cha kisasa zitakazo wasaidia kuongeze uzalishaji na kupata mavuno mengi.


Mkulima na Mwanachama wa Chama hicho Gisat Komba alisema,kwa muda wa miaka minne uzalishaji wa kahawa umeongezeka na hali hiyo imetokana na upatikanaji wa pembejeo za ruzuku zinazotolewa na Serikali ambazo zimehamasisha watu wengi hasa vijana kujikita kwenye kilimo cha zao hilo.

Hata hivyo alisema,changamoto kubwa ni soko la uhakika kwani wanunuzi wana tabia ya kujipangia bei ya kahawa bila kuwashirikisha wakulima jambo linalowaumiza sana kwa sababu wanatumia gharama kubwa katika uzalishaji wake.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa kata ya Utiri Libaba Gervas Libaba alisema,kata hiyo ni maarufu kwa kilimo cha zao la kahawa na Wananchi wanajitahidi sana kulima,lakini changamoto iliyopo ni upatikanaji wa pembejeo za ruzuku.

Ametoa ombi kwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara za mijini na vijijini(Tarura) Wilaya ya Mbinga,kukamilisha ujenzi wa Barabara ya lami ya Utiri-Mahende kwa kiwango cha lami ili iweze kusaidia wakulima kusafirisha mazao kupeleka sokoni kwa haraka kwani barabara hiyo inapita kwenye maeneo yenye uzalishaji mkubwa wa kahawa.


No comments:

MAKAMU WA RAIS DKT. PHILIP MPANGO AWATAKA WATANZANIA KUKEMEA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

  Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawak...