Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, amewasili nchini Barbados kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa Kimataifa kuhusu matumizi ya Nishati Endelevu. Mkutano huo unatarajiwa kufanyika katika jiji la Bridgetown kuanzia tarehe 12 hadi 14 Machi 2025, ukiwaleta pamoja wadau wa sekta ya nishati kutoka mataifa mbalimbali duniani.
Mhe. Dkt. Biteko alipowasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Grantley Adams, alipokelewa na Waziri wa Nishati wa Barbados, Mhe. Lisa Cummins, pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Cuba na mwakilishi katika eneo la Karibiani, Mhe. Humphrey Polepole.
Katika mkutano huo, Dkt. Biteko atashiriki majadiliano muhimu yanayohusu matumizi ya Nishati Endelevu duniani, akijikita zaidi katika kuhimiza upatikanaji wa Nishati Safi ya kupikia. Ajenda hii ni ya msingi kwa maendeleo endelevu na inalenga kuwaondoa wananchi, hususan wa nchi zinazoendelea, kutoka kwenye matumizi ya nishati duni ambayo si rafiki kwa afya wala mazingira.
Mbali na kushiriki majadiliano, Dkt. Biteko pia anatarajiwa kuwasilisha mtazamo wa Tanzania kuhusu uwekezaji katika sekta ya nishati, akisisitiza fursa zilizopo kwa wawekezaji wa kimataifa kushirikiana na Tanzania katika kufanikisha mipango ya nishati safi na endelevu.
Katika safari hii, Dkt. Biteko ameambatana na Mshauri wa Rais wa Masuala ya Wanawake, Mhe. Angellah Kairuki, Waziri wa Maji, Nishati na Madini wa Zanzibar, Mhe. Shaib Hassan Kaduara, pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felichesmi Mramba. Ujumbe huu wa Tanzania unatarajiwa kushiriki kikamilifu katika mijadala, mikutano ya uwekezaji, na mazungumzo ya ushirikiano wa kimataifa ili kuimarisha sekta ya nishati nchini.
Mkutano huu wa kimataifa unatarajiwa kuwa jukwaa muhimu kwa Tanzania katika kujitangaza kama miongoni mwa nchi zinazojizatiti katika kuwekeza kwenye nishati endelevu, huku ikihamasisha ushirikiano wa kimataifa katika kufanikisha ajenda ya nishati safi kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
No comments:
Post a Comment