Friday, March 14, 2025

ALMASI, DHAHABU ZAIPAISHA SHINYANGA






🟠*Yafikia 82% ya lengo ukusanyaji maduhuli*


·  Fursa bado zipo njooni - Mapunda

MAKUSANYO  ya maduhuli ya Serikali kupitia Sekta ya Madini katika Mkoa wa Shinyanga  yatokanayo na mrabaha, tozo na ada mbalimbali kwa mwaka wa fedha  ulioanza Julai 2024/ 2025 ni Shilingi Bilioni 21.5

 Mkoa wa Shinyanga ulipangiwa kukusanya Shilingi Bilioni 26.2 ambapo mpaka mwishoni mwa mwezi Februari mwaka huu  umefanikiwa kukusanya kiasi hicho cha fedha ambacho ni sawa na asilimia 123 katika kipindi cha miezi nane na asilimia 82 ya lengo la mwaka.

Akizungumza katika mahojiano maalum, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Mjiolojia Daniel Mapunda amesema fedha hizo zimekusanywa kutokana na  jitihada mbalimbali walizofanya katika usimamizi wa sekta.

 “Mwenendo ni mzuri, hadi kufikia mwisho wa mwaka wa fedha tuna imani tutafikia lengo,” amesema Mapunda.

Aidha, Mapunda ametoa wito kwa wawekezaji kote nchini kuchangamkia fursa za uwekezaji zilizopo katika Sekta ya Madini mkoani Shinyanga ambao una utajiri mkubwa wa madini ya Almasi, Dhahabu na Madini Ujenzi.

“Mkoa wa Shinyanga tuna shughuli mbalimbali za madini ambazo zinajumuisha utafiti, uchimbaji, uchenjuaji na biashara ya madini;…. “Shughuli hizi zinafanyika kwenye wilaya zote mbili, Kishapu na Shinyanga.

“Tuna migodi mikubwa miwili wa kati mmoja na leseni 375 za uchimbaji mdogo na katika kipindi cha mwaka wa fedha 2024/ 2025 tumetoa leseni ndogo za biashara ya madini  51 na leseni kubwa za biashara ya madini 21 amesema Mapunda.

Amesema,  pia zipo fursa  za uchenjuaji wa madini na kwamba wana  jumla ya mitambo 150 ya uchenjuaji katika maeneo yanayosimamiwa na Tume ya Madini katika Wilaya za Kishapu na Shinyanga.

Amesema Mkoa wa Shinyanga una soko kuu la madini moja na vituo vitano vya ununuzi wa madini katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri za wilaya za Shinyanga na Kishapu

Katika hatua nyingine, Mapunda amesema kuwa  kutokana na elimu kuhusu wajibu wa wamiliki wa miradi ya madini kuchangia miradi ya maendeleo ya jamii kutolewa mara kwa mara na ofisi yake, matokeo makubwa  yameonekana ikiwa ni pamoja na kuongezeka kwa mwamko kwa wachimbaji wadogo  wa madini kwenye uchangiaji wa uboreshaji wa huduma za jamii ikiwa ni pamoja na shule na vituo vya afya tofauti na miaka ya nyuma ambapo uchangiaji ulikuwa unafanywa na migodi mikubwa na ya kati tu.

Amefafanua kuwa, jumla ya miradi ya uchimbaji mdogo 21 na miradi ya uchenjuaji mitano imeshirikishwa na kuwekwa kwenye mpango wa uchangiaji wa miradi ya maendeleo ya jamii  katika Halmashauri  za wilaya za Kishapu na Shinyanga kwa kipindi cha mwaka ujao wa fedha 2025/ 2026.

“ Kwa migodi mikubwa na ya kati katika mkoa wa Shinyanga imeendelea kufanya vizuri katika eneo la ushirikishwaji wa watanzania katika Sekta ya Madini ambapo mpaka sasa zaidi ya asilimia 90 ya manunuzi ya bidhaa, vifaa na huduma ni ya ndani tofauti na miaka ya nyuma, amesisitiza Mapunda.

No comments:

PAC YAIPONGEZA MSD KWA KUJENGA GHALA LA KISASA LA KUHIFADHIA BIDHAA ZA AFYA

Na Mwandishi Wetu. Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) chini ya Mwenyekiti wake, Mhe. Naghenjwa Kaboyoka (pichani) imetemb...