Mkurugenzi wa Halmasahuri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda (wa kwanza kushoto) akisoma taarifa ya vifaa vilivyokabiidhiwa kutoka UNICEF
Sehemu ya watoto wenye mahitaji maalumu kutoka shule ya Msingi Ramadhani, Kibena na Kituo cha Kulelea watoto Yatima cha Compassion waliofika kwenye makabidhiano hayo
Msaada wa Vifaa kwa watoto wenye mahitaji maalumu kutoka UNICEF
Mtoto mwenye ulemavu wa macho Timoth Mwageni akitoa shukrani zake kwa UNICEF mara baada ya kupokea misaada hiyo.
Hyasinta Kissima-Njombe.
Shirika la kulinda na kutetea haki za watoto dunia UNICEF limetoa vifaa vya aina mbalimbali vyenye thamani ya Shilingi Milioni 4,591,000/= kwa makundi matatu ya watoto wenye mahitaji maalumu katika Halmashauri ya Mji Njombe.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda amesema kuwa anaipongeza UNICEF kwani wamekuwa wadau wakubwa wa maendeleo katika halmashauri yake sio kwa upande wa lishe kwa watoto bali hata kujali makundi ya watoto wenye mahitaji maalumu.
Aidha Mkurugenzi huyo amevipongeza vyombo vya habari kwa kuandika habari mbalimbali za kijamii kwani kupitia habari za shughuli za kijamii zilizokuwa zinaandikwa na vyombo vya habari shirika la UNICEF liliguswa na kuona ni vyema kuunga mkono jitihada hizo.
“Ninaamini kabisa Kwa jitihada za waandishi wa habari kutangaza habari ambazo huwa tunatoa misaada kidogo kidogo ile ya Halmashauri kila robo ya mwaka kwa vituo mbalimbali vya kulelea watoto habari ziliwafikia wenzetu wa UNICEF nao wakaona ni vizuri wakatuunga mkono”Alisema Mwenda.
Farida Mgeni ni mzazi ambaye mtoto wake wa umri wa miaka sita anaulemavu wa akili ambaye yeye ameishukuru UNICEF kwa kupokea msaada wa godoro, mashuka, blanket na vifaa vya kuchezea mtoto wake na amesema vifaa hivyo vitamsaidia sana mtoto wake alikua hana malazi na vifaa vya michezo vitaendelea kuimarisha akili na kuongeza uchangamfu kwa mtoto wake.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Hosea Yusto amesema kuwa miongoni mwa changamoto wanazokumbana nazo katika kutambua uwepo wa watoto wenye mahitaji maalumu ni pamoja na wazazi kutokuwa na uelewa kuwa licha ya mtoto kuwa na ulemavu bado anahaki ya kupata mahitaji yake yote ya msingi na hivyo kupelekea watoto kufichwa ndani bila kupatiwa huduma kama elimu na afya na amewataka wazazi kuachana na tabia hiyo na kuhakikisha watoto hao wanatambuliwa ili waweze kupatiwa huduma wanazostahili.
Vifaa vilivyokakabidhiwa ni pamoja na magodoro, mashuka, blanket, vifaa maalumu vya kujifunzia na vifaa vya michezo Halmashauri ya Mji Njombe inajumla ya vituo vitatu vyenye waalimu waliopatiwa elimu maalumu ya jinsi ya kuwafundisha watoto wenye ulemavu.
No comments:
Post a Comment