Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ameridhia ombi la Rais wa Uganda Yoweri Museveni la kuweka bomba la kupitisha gesi kutoka Mtwara kwenda Uganda, baada ya ujenzi wa bomba kukamilika.
Akihutubia wananchi wakati wa sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kusafirisha mafuta kutoka Uganda mpaka Tanzania Hoima, Rais Magufuli amesema haitakuwa sahihi kuwanyima Uganda gesi wakati wao wanaleta mafuta kwenye bandari ya Tanga.
“Kutoka Msimbati Mtwara mpaka Uganda kuna kilomita 1422, kwa hiyo kuweka bomba ambalo litapitisha gesi wakati hili lingine linapitisha mafuta, inashindikana nini? Napenda kumuhakikishia muheshimiwa haya yanawezakana, bomba la gesi lipite hapa kwenda Uganda, Kama wao wametukubalia kwa nini sisi tushindwe, huu ndio ushirikiano wa Afrika Mashariki , Tuwapelekee gesi wakafufue viwanda vyao vya chuma kule”, alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli aliendelea kusema kuwa kitendo hicho kitakuwa kinatekeleza kanuni ya ushirikiano wa Afrika Mashariki, na kuweza kukuza uchumi kwa pamoja.
Ombi la Uganda kupelekewa gesi ilitolewa na Rais wa Uganda Mh. Yoweri Museveni alipokuwa akizungumza na Watanzania, na kusema nchi ya Uganda ina madini ya chuma, lakini haina gesi ya kuweza kuendesha viwanda vya kufua vyuma hivyo, kwa hiyo akaiomba serikali ya Tanzania iweze kusaidia katika hilo.
No comments:
Post a Comment