Friday, February 26, 2010

Serena kujenga shule nyingi Afrika








NAIROBI, Kenya

MCHEZA tenisi namba moja katika ubora wa wachezaji tenisi wanawake duniani anayetokea Marekani Serena Williams amesema ana mpango wa kusaidia kujenga shule moja mpya katika sehemu mbalimbali za Afrika kila mwaka ili kuweza kuwasaidia watoto wa Afrika.

Serena ambaye hivi sasa yupo Barani Afrika kwa ajili ya miradi mbalimbali ya kijamii akiwa balozi wa kampuni ya HP ambayo inatengeneza kompyuta na vifaa vingine vya kiteknolojia, amesaidia ujenzi wa shule nchini Kenya, Senegal na Afrika Kusini, pia amesaidia kulipa ada za wanafunzi na amejiunga katika mpango wa kutokomeza malaria nchini Ghana.

"Ni dhamira yangu kufungua shule nyingi kwa ajili ya maelfu ya wanafunzi barani Afrika ambao hawajapata nafasi ya kwenda shule kupata elimu. Nimepanga kujenga shule moja kila mwaka,"alisema Serena mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wa ziara yake ya siku tatu nchini Kenya, ambapo alifungua shule ya sekondari huko Makueni kilomita 150 kusini mashariki ya Nairobi.

Kabla ya ziara hii barani Afrika, Serena alishawahi kwenda Kenya mwaka 2008 na kufungua shule katika eneo hilo hilo la Kusini mashariki ya Kenya, eneo ambalo kwa muda mrefu limekuwa likitegemea chakula cha msaada kwa sababu ya ukame.

"Bila elimu, maisha yanakuwa magumu. Wazazi wangu kila siku walikuwa wakisisitiza umuhimu wa kupata elimu, natumai nimeleta matunda ya maneno yao kwa mimi kupata elimu na kuja hapa Kenya kufungua shule hii ya Wee,"alisema Serena Williams wakati akifungua shule ya sekondari inayoitwa 'Serena Williams Wee Secondary School.'

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...