Friday, February 19, 2010

Bomani aishangaa serikali kuogopa mgombea binafsi

Asema baba wa taifa Mwalimu Nyerere alibariki hilo mwaka 1995


MWANASHERIA Mkuu wa Kwanza mzalendo nchini, Jaji Mark Bomani amesema serikali inakwamisha bila sababu suala la mgombea binafsi katika uchaguzi, ambalo licha ya kupata baraka za mahakama lilishapata baraka zote za baba wa taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Mbali na kuitaka serikali kuacha kigugumizi katika kuruhusu utekelezaji wa suala hilo; alikosoa mfumo wa sasa wa uchaguzi na uteuzi wa mawaziri na kupendekeza kwamba, siyo lazima waziri awe mbunge.

Suala hili lilifunguliwa kesi katika Mahakama Kuu ya Tanzania na Mwenyekiti wa DP, Christopher Mtikila ambayo ilitoa hukumu mwaka 2006 iliyoruhusu kuwepo mgombea binafsi, lakini serikali imeendelea kuweka ngumu kwa kukata rufaa katika Mahakama ya Rufaa kuomba hukumu hiyo ipitiwe upya.
Februari 8, mwaka huu Jaji Mkuu, Augustine Ramadhan aliahirisha kusikiliza rufaa hiyo baada ya ofisi ya Mwanasheria Mkuu kutojiandaa vizuri hivyo kuomba isogezwe mbele. Akiahirisha rufaa hiyo, Jaji Ramadhan alisema hukumu ya Mahakamu Kuu itaendelea kama ilivyo hadi hapo rufaa itakapopitiwa na jopo la majaji wa Mahakama ya Rufaa na kumlaumu Naibu Mwanasheria Mkuu kwa kutojiandaa kikamilifu wakati wao ndiyo walioomba ipitiwe upya.

Katika taarifa yake maalumu aliyoitoa kwa gazeti hili jana, Jaji Bomani alisema mfumo wa mgombea binafsi katika chaguzi sio haramu kwa kuwa umeshakubaliwa na wataalamu mbalimbali.

Kauli hiyo ya Jaji Bomani imekuja karibu majuma mawili tangu jopo la majaji saba wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuitaka serikali kuwa makini katika rufaa waliyoikata dhidi ya hukumu ya mahakama kuu kuwepo kwa mgombea binafsi.

Walisema endapo serikali italegalega katika rufaa yake dhidi ya hukumu hiyo iliyotolewa na Mahakama Kuu ya Tanzania, suala la kuruhusiwa mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu ujao, liko palepale.

Jaji Bomani ambaye alishawahi kushiriki katika kamati mbalimbali za kutafiti mfumo sahihi wa uchaguzi unaofaa Tanzania, alitoa changamoto kwa Rais Jakaya Kikwete kuwa ndiye anayepaswa kusimamia suala hilo.

Alisema Rais Kikwete ana nguvu na nafasi ya kihistoria kutekeleza uamuzi huo wa mahakama kwa kuruhusu mgombea binafsi katika uchaguzi mkuu ujao.

Jaji Bomani alisema hatua nzuri na muhimu ya kuanzia katika utekelezaji wa suala la mgombea binafsi na kuboresha mfumo wa uchaguzi Tanzania, ni kupitia upya ripoti ya Jaji Kisanga, jambo alilosema kuwa serikali haijachelewa.
Imeandikwa na Salim Said na Nora Damian: SOURCE:MWANANCHI

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...