Friday, February 05, 2010

Breaking Newssss Jerry Muro Kizimbani

JESHI la Polisi limemfikisha mahakamani mwandishi wa habari , Jerry Muro, ambaye ni maarufu kwa kufichua uozo, baada ya kumkamata kwa tuhuma za kudai rushwa kwa nguvu.

Kafikishwa katika mahakama ya Kisutu asubuhi hii watu kibao wamemiminika kushuhudia tukio hilo lililogusa hisia za watu wengi.

Muro, mfanyakazi wa Shirika la Utangazaji (TBC), anadaiwa kutaka fedha kwa njia ya vitisho kutoka kwa mhasibu aliyesimamishwa wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage.Taarifa zaidi tutawaleteeni baadaye.

----------------------------------------------------------------------------------

Jerry Muro apandishwa kizimbani

HATIMAYE mtangazaji wa kituo cha televisheni cha Shirika la Utengazaji (TBC1), Jerry Muro jana alipandishwa kizimbani akishtakiwa kwa mashtaka ya kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni.
Muro, ambaye ni mtangazaji wa kipindi maarufu cha Usiku wa Habari cha televisheni hiyo ya serikali, alifikishwa kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana baada ya kukamatwa Jumapili iliyopita katikati ya jiji la Dar es salaam.
Mtangazaji huyo, ambaye alichomoza kutokana na kuripoti habari zilizofichua rushwa inayofanywa na askari wa kikosi cha usalama barabarani, alipandishwa kizimbani akiwa na wenzake wawili ambao inadaiwa alishirikiana nao katika kutenda kosa hilo. Wawili hao walisomewa mashtaka matatu.
Washtakiwa hao wote walifikishwa mahakamani hapo wakiwa chini ya ulinzi mkali wa askari waliokuwa wamevalia nguo za kiraia.
Muro ameunganishwa na watu hao katika shtaka la kula njama na kuomba rushwa ya Sh10 milioni, lakini wawili hao walisomewa mashtaka mengine matatu ya kujifanya wafanyakazi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Wakili mwandamizi wa serikali, Boniface Stanslaus akishirikiana na mwendesha mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Ben Lincoln waliwataja washtakiwa wengine waliopandishwa kizimbani na Muro kuwa ni Edmund Kapama, maarufu kama Doctor, na Deogratias Mgasa ambaye ni maarufu kama Musa.
Stanslaus, ambaye aliisoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Gabriel Mirumbe, alidai kuwa Muro na wenzake walikula njama na kuomba rushwa ya fedha hizo mwezi Januari, jambo ambalo alisema ni kinyume cha kifungu cha 15 (1)(a) cha Sheria ya Kuzia ya Kupambana na Rushwa ya mwaka 2007.
Wakili Stanslaus alidai katika shtaka la pili kuwa Januari 29 mwaka huu katika hoteli ya Sea Cliff wilayani Kinondoni, Jerry Muro, akiwa mwajiriwa wa TBC1, aliomba rushwa ya Sh10 milioni kutoka kwa mhasibu wa zamani wa Halmashauri ya Bagamoyo, Michael Wage Karoli.
Alidai Muro aliomba kiasi hicho cha fedha ili asitangaze habari za Kalori zinazohusu matumizi mabaya ya fedha za umma.
Kwa sasa Wega, na wafanyakazi wengine watatu wa halmashauri hiyo, amesimamishwa kazi kutokana na tuhuma za matumizi mabaya ya fedha za umma. Alisimamishwa kazi na Waziri Mkuu Mizengo Pinda alipotembelea wilaya hiyo baada ya ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Serikali (CAG) kuonyesha mapungufu makubwa kwenye matumizi ya fedha.
Katika shtaka la tatu, Stanslaus alidi kuwa siku ya tukio washtakiwa Edmund Kapama na Deogratias Mgasa walijipachika nyazifa zisizokuwa zao.
Aliongeza kudai kuwa washtakiwa hao wakiwa katika hoteli hiyo ya Sea Cliff walimlaghai Wega kwa kuwa wao ni maofisa wa Takukuru huku wakijua ni uongo.
Baada ya kumaliza kuwasomea mashtaka hao, washtakiwa wote walikana na upande wa mashtaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.
Hakimu Mirumbe aliwaachia huru washtakiwa Jerry Muro na Edmund Kapama baada ya kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa.
Washtakiwa hao waliachiwa mara baada ya kila mmoja kusaini dhamana ya Sh5 milioni na wadhamini wawili, kila mmoja akisaini dhamana ya kiasi hicho cha fedha.
Mshtakiwa wa tatu, Mgasa alirudishwa rumande kwa kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.
Muro aliondoka mahakamani hapo saa 7:38 mchana akiwa kwenye gari aina ya Toyota RAV 4 lenye namba za usajili T607 ANM.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Februari 10 mwaka huu.
Katika kesi hiyo Muro anatetewa na wakili Pascal Kamala

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...