Wednesday, February 17, 2010

'Haturidhiki na uamuzi wa bunge kuhusu Richmond'



WANAHARAKATI wa FemAct na vikundi vingine vya kiraia nchini wameeleza kutoridhishwa na kushtushwa na utendaji wa Bunge na Wabunge baada ya kushindwa kuchukua hatua madhubuti dhidi ya kashfa ya Richmond na nyingine.

Kutokana na hatua hiyo wananaharakati hao, wametangaza kuandaa maandamano nchi nzima kuonyesha kutoridhishwa na utendaji wa Bunge.
Aliema wananchi watahamasishwa kuonyesha hasira dhidi ya chombo hicho na kudai mfumo mbadala wa demokrasia nchini.

Wakitoa tamko la pamoja lililoshirikisha asasi na vyama vya kiraia zaidi ya 50, makao makuu ya Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP) jijini Dar es Salaam, wanaharakati hao wamelitaka Bunge kujisafisha kwa kuweka maslahi taifa mbele badala ya maslahi ya vyama na wabunge binafsi.

“Tofauti na matarajio ya wananchi, Bunge limemaliza kikao chake bila kuchukua hatua madhubuti kuhusu kashfa ya Richmond, Kiwira, Ticts, TRL, Loliondo na North Mara. Jambo hili limetushtua na kutusikitisha sana,” alisema Kaiza Buberwa mkurugenzi wa asasi ya Fordia.

“Sisi wananchi tunanona kuwa Bunge limeshindwa kutekeleza wajibu wake kikatiba wa kuisimamia serikali, kutokana na mfumo mbaya wa madaraka na uwajibikaji kati ya serikali na bunge unaoruhusu maslahi ya chama tawala kuchukua hatamu kuliko maslahi ya taifa,” alisema Buberwa.

“Tunapendekeza Bunge lijisafishe na kuweka maslahi ya taifa mbele kuliko maslahi ya vyama na wabunge binafsi,” alisema mkurugenzi wa kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Francis Kiwanga.

“Kama Asasi za kiraia tumeamua kuandaa maandamano makubwa ya kitaifa kuonyesha kutoridhishwa na utendaji usioridhisha wa Bunge la sasa na kudai mfumo mbadala wa demokrasia shirikishi ambao una uwezo zaidi kutetea maslahi ya wananchi,” alisema.

Wanaharakati hao walibainisha kuwa fedha zilizopotea katika kashfa ya Richmond zinazofikia Sh173 bilioni zingeweza kutosha kujenga nyumba19,211 za walimu wa shule ya msingi huku kila shule ikigharimu Sh9 milioni.

Walisema kutokana na mfumo uliopo hivi sasa, ni vigumu Bunge kuiwajibisha serikali na ndiyo sababu Bunge limefunika kisiasa kashfa za Richmond, mgodi wa makaa ya mawe Kiwira, TRL na Ticts. Imeandikwa na Exuper Kachenje: SOURCE -MWANANCHI

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...