Hatimaye mfungwa atunukiwa shahada gerezani








HARUNA Pembe Mgombela (54) pichani juu, ambaye ni mfungwa katika Gereza la Ukonga, jijini Dar es Salaam jana alikabidhiwa rasmi cheti cha kuhitimu shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu Huria Tanzania aliyosoma akiwa gerezani humo.

Pamoja na kukabidhiwa shahada hiyo kwenye mahafali maalum yaliyofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Maafisa Magereza Ukonga, Mgombela alisema yuko tayari kuendelea na masomo ya juu ya Shahada ya Uzamili, kama alivyoahidiwa na kupata udhamini wa Chuo Kikuu hicho.

Mgombela alisema ahadi hiyo iliyotolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Huria, Profesa Tolly Mbwette baada ya kumkabidhi rasmi cheti hicho ni changamoto kwake hivyo ataitumia vyema nafasi hiyo.

"Niko tayari kuanza shahada ya uzamili hata leo, siwezi kukata tamaa, nia yangu kubwa ni kujiendeleza na kutumia fursa hii vizuri huku nikiendelea kutumikia adhabu yangu kujirekebisha kwa mujibu wa sheria," alisema Mgombela, mzaliwa wa Kibaha mkoani Pwani.

Aliongeza kuwa matarajio yake kwa sasa ni kuendelea kujiandaa akiwa gerezani na kutumia taaluma hiyo kuwasaidia wafungwa wenzake katika masuala ya kisheria, hasa baada ya kutoa ushauri na kuandika hati za rufaa zilizowawezesha wafungwa zaidi ya 90 kushinda rufaa zao.

Alisema kwa sasa si rahisi kwake kufikiria hatma yake baada ya kutoka gerezani kwa kuwa bado ana muda mrefu wa takribani miaka 25 anayotakiwa kuitumikia katika gereza hilo ikiwa ni sehemu ya adhabu ya miaka 50 aliyohukumiwa.

Mgombela alisema katika muda wote wa masomo yake tangu alipojiandikisha rasmi mwaka 2004, hakuwahi kutoka gerezani humo kwa ajili ya shughuli yoyote ya kujisomea, lakini alikuwa akipata nafasi ya kutembelea maktaba ya gereza hilo na kupelekewa vitabu alivyohitaji.

Picha ya Faraja Jube na imendikwa na Andrew Msechu wa Mwananchi

Comments