Saturday, September 29, 2007

Tamko la Serikali Kwa Slaa

SERIKALI imetoa taarifa kujibu shutuma za rushwa kwa viongozi na watendaji wakuu wa serikali zilizotolewa na Mbunge wa Karatu kwa kupitia CHADEMA Dk. Wilbrod Slaa hivi karibuni.

Taarifa hiyo iliyotolewa Ijumaa Sept. 28, 2007 na Waziri ya Habari, Utamaduni na Michezo Mh. Muhammad Seif Khatib imesema shutuma hizo hazina msingi wowote na zinastahili kupuuzwa.

"Tafsiri pekee na mantiki ya kutolewa kwa tuhuma hizi wakati huu ni kuwa hili ni jaribio la kuwavunja moyo wananchi kuhusu manufaa ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005," imeeleza.

Imesema kwmba Serikali inapinga vitendo vya rushwa nchini "kwa nguvu zake zote" na kama Dk. Slaa na wenzake wana lengo la kupiga vita rushwa basi tuhuma hizo wangezifikisha katika vyombo vinavyohusika ili zishughulikiwe.

Dk. Slaa, akiwaongoza wanasiasa wenzake kadhaa wa kambi ya upinzani, walitoa tamko hadharani Septemba 15 mwaka huu kwenye viwanja vya Mwembeyanga, wilaya ya Temeke, mkoani Dar es Salaam, kuwatuhumu viongozi kadhaa wa umma kuwa wanashiriki vitendo vya rushwa.

Kufuatia tuhuma hizo, gazeti la kila wiki la MwanaHalisi linalotolewa jijini Dar es Salaam, limekuwa likisambaza tuhuma hizo bila ya kutafuta ukweli wake, taarifa imesema.

Taarika kamili ya Serikali inatarajiwa kuchapishwa ikiwa ni tangazo katika magazeti kadhaa ya kila siku Jumamosi Sept. 29, 2007.

Taarifa imesema Serikali ya Tanzania wakati wote imekuwa ikitekeleza mipango na mikakati mbalimbali ya kupambana na rushwa, awamu ya kwanza ya mwaka 1997/2004 na awamu ya pili mwaka 2005/2010.

Imenukuu Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, Ibara ya 110, inayoelezea mapambano dhidi ya rushwa na tamko la Rais Jakaya Kikwete dhidi ya rushwa katika hotuba yake ya kuzindua Bunge Desemba 29, 2005.

Serikali imeanzisha Ofisi za Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwenye Wilaya zote nchini, imeshughulikia taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na inashirikisha wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa, imesema.

"Serikali isingebuni na kutekeleza mikakati hii kama isingekuwa na nia ya dhati ya kupambana na tatizo la rushwa [WINDOWS-1252?]nchini…Serikali haikutarajia kwamba watakuwepo miongioni mwetu watakaotumia fursa hizi kuibua taarifa za uzushi kwa lengo la kuchafua majina ya wenzao ili kujipatia umaarufu wa kisiasa wasioustahili," imeongeza.

Taarifa imesema Serikali inaelewa kwamba Dk. Slaa na wenzake ni miongoni mwa viongozi walioshiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2005 wakitegemea kushinda lakini walishindwa na wananchi kuichagua CCM.

Imesema wananchi wanayaona mafanikio mengi katika utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kwamba wanachokitafuta wale walioshindwa ni kile walichokikosa na hivyo wanajaribu kuwahadaa na kuwachanganya wananchi.

"Serikali ya Awamu ya Nne ni imara na iko makini kutekeleza ahadi zake zote ilizowaahidi wananchi wakati ilipokuwa inawaomba ridhaa ya kuingia madarakani.

"Hivyo ni vyema wananchi wakatambua kwamba wapinzani hawa hivi sasa wanatapatapa na wanataka kutuondoa katika lengo letu la kuwaletea maisha bora Watanzania," imeongeza.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...