Tuesday, September 25, 2007

Mudhihir atolewa Muhimbili



MBUNGE wa Mchinga, Mudhihir Mohamed Mudhihir, ameruhusiwa na madaktari kutoka Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) baada ya hali yake kuonekana inaendelea vizuri.

Akuzungumza na waandishi wa habari katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili jijini Dar es Salaam jana, daktari wa mbunge huyo, Paul Marealle, alisema kuwa, wamemruhusu baada ya kuona anaendelea vizuri bila ya matatizo yoyote.

Daktari huyo aliongeza kuwa moja ya masharti waliyompa ni kwenda hospitali kufunga kidonda kila baada ya siku moja.

"Mbunge tumemruhusu baada ya kuona hali yake inaendelea vizuri tofauti na awali alivyoletwa. Tuna matumaini hata atakapokuwa nyumbani atakuwa anaendelea vizuri tu bila matatizo yoyote," alisema Marealle.

Wakati huo huo; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samwel Sitta aliliambia gazeti hili kwa simu jana kuwa, Bunge lina wajibu wa kumuhudumia mbunge huyo tangu alipopata ajali hadi mwisho.

Sitta alisema kuwa, wameandaa mazingira ya kumpeleka Mudhihir nchini Ujerumani kwa ajili ya matibabu zaidi.

"Mpaka sasa hivio wabunge wote wanatambua kwamba mbunge mwenzao anaumwa na wako tayari kushirikiana naye atakapopelekwa Ujerumani kwa ajili ya matibabu zaidi.

"Katika safari hiyo ataambatana na mbunge mmoja ambaye atamsindikiza. Kwa sasa tunasubiri gharama za matibabu zitakazoletwa na madaktari kutoka Ujerumani kwa faksi ili kufahamu gharama zinazotakiwa kumuhudumia kabla ya yeye kwenda huko," alisema Sitta.

Kwa mujibu wa Sitta, Mudhihir atatarajiwa kuanza safari ya kwenda Ujerumani kwa matibabu ndani ya siku mbili zijazo. Kuanzia jana na leo, madaktari wa MOI na wa Ujerumani wanashirikiana kupata hospitali ambayo atapelekwa.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...