Tuesday, September 25, 2007

Prof Kapuya Chupu Chupu








Waziri wa ulinzi na jeshi la Kujenga Taifa, Profesa juma Othman Kapuya, amenusurika
katika ajali mbaya ya gari ambayo pia ilipoteza maisha ya walinzi wake wawili pamoja
na diwani wa kata ya Ushokola wilayani Urambo.

Kwa Mujibu wa mkuu wa mkoa wa Tabora, Bw Abeid Mwinyimsa na kamanda wa polisi
mkoani Tabora, Muhud Mshihiri, ajali hiyo ilitokea katika kijiji Usindi kata ya
Kaliua.

Taarifa hiyo imesema kuwa kijiji hicho kiko umbali wa kilomita nane kutoka katika
makao makuu ya kata hiyo mjini Kaliua, ambako ndiko nyumbani kwa Waziri Kapuya.

Watu watatu waliofariki katika ajali hiyo ni pamoja na walinzi wawili wa Profesa
Kapuya, ambao ni askari jeshi na diwani wa kata ya Ushokola wilayani Urambo, ambaye
alikuwa amfuatana na kiongozi huyo katika ziara yake ya kuhimiza maendeleo.

Mlinzi mmoja, Ramadhan Mlini, alifariki papo hapo hapo pamoja na diwani Haruna
Shamsheri, huku mlinzi mwingine Shaaban akifariki muda mfupi baada ya
kufikishwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

watu wengine wanne waliokuwa kwenye gari hiyo, ambao wamepata majereha ni pamoja na
mwenyekiti wa CCM wa wilaya ya Urambo Twaha Ngosso, msaidizi wa waziri huyo Luteni
Kanali Leopald Kalima, dereva wa gari hiyo Christopher Charles mwenye namba MT 57185
na mfanyabiashara Shigela Mabula.

Taarifa za awali kuhusu ajali hiyo zinasema kuwa chanzo chake ni kupasuka kwa
gurudumu la mbele la upande wa kulia na hivyo kupinduka.

Waziri kapuya, amelazwa katika hospitali ya wilaya ya Urambo mkoani Tabora, pamoja
na majeruhi wengine wanne, huku mipango ya kuhakikisha kuwa anapata tiba bora zaidi
ikiendelea kufanywa.

Waziri Kapuya, alikuwa katika ziara ya kuhamasisha maendeleo katika jimbo la Urambo
Magharibi, akitoka katika kijiji cha Kashishi kilomita zaidi ya 100 kutoka makao
makuu ya jimbo hilo mjini Kaliua.

No comments:

WIZARA YA ARDHI YAPONGEZWA KUTENGA FEDHA KUKAMILISHA MRADI WA MAKTABA

Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii imeipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kutenga fedha kiasi cha Shiling...